Magufuli aeleza sababu kuwashwa Mwenge wa Uhuru

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru mwaka 1961 ilikuwa ishara ya ukomo wa dhuluma, dharau na uonevu vilivyokuwa katika utawala wa wakoloni.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru mwaka 1961 ilikuwa ishara ya ukomo wa dhuluma, dharau na uonevu vilivyokuwa katika utawala wa wakoloni.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Oktoba 14, 2019 wakati akihutubia katika maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere yaliyofanyika mkoani Lindi.

Rais Magufuli amesema hiyo ilikuwa ishara ya mwangaza na matumaini mapya kwa Taifa.

Amesema mwalimu Nyerere aliamini uhuru wa Tanzania usingekuwa na maana endapo mataifa mengine yangebaki chini ya utawala wa kikoloni.

Ameeleza kuwa dhamira hiyo ya Baba wa Taifa ndio ilisaidia  harakati za ukombozi katika nchi nyingine zilizo Kusini mwa Afrika.

“Ndio maana Oktoba 1959 mwalimu Nyerere alitamka namnukuu, ‘sisi Watanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau’,” amesema Magufuli.

Amesema Mwenge uliwekwa juu ya Mlima Kilimanjaro ili mwanga wa matumaini usiishie Tanzania peke yake, bali  usambae kwenye mataifa mengine Kusini mwa Afrika kufanikisha ukombozi.

“Mwalimu Nyerere aliamua Taifa letu kuwa kitovu cha harakati za ukombozi na nchi yetu ilishiriki kikamilifu katika ukombozi wa Bara la Afrika,” amesema Rais Magufuli.