Magufuli aelezea jinsi urais ulivyo mgumu

Muktasari:

  • Rais Magufuli aeleza jinsi kazi ya urais ilivyokuwa ngumu, lakini asema ataendelea kutimiza wajibu wake kwa sababu ana imani Mungu na Watanzania ndio waliompa nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameeleza namna ambavyo kazi ya urais ilivyokuwa ngumu kutokana na changamoto mbalimbali zinavyoendelea kujitokeza.

Amesema hayo leo Jumapili Aprili 7, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa Mbinga mkoani Ruvuma baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa kilomita 67 yenye thamani ya Sh134.712bilioni.

Rais Magufuli amewaambia wakazi hao kuwa “Urais ni mgumu, tena mgumu kweli. Hupati muda kupumzika, unakuja huku unajua umechoka lakini mafaili yanakufuata tena yameandikwa ni muhimu.”

“Mara usiku unapigiwa simu na fulani au  rais wa nchi fulani na yeye anakupigia simu. Lakini lazima tufanye kwa sababu ninaamini Mungu pamoja na Watanzania ndio walionipa hii nafasi.”

Ameendelea kuwaeleza kuwa, “Nitatumika kama sadaka yangu kwa wananchi wa Tanzania. Ndio maana siku zote nimekuwa nikisisitiza mniombee na msichoke, lakini msichoke kuwaombea viongozi hawa wakiwemo mawaziri wangu.”

Amesema mawaziri wa awamu ya tano wana shida na kupata nafasi katika utawala wake ni mateso kwa sababu huna uhakika kama utamaliza nafasi yako bila kuondolewa, tofauti na miaka iliyopita.

“Enzi zetu ukiteuliwa uwaziri unajua hakika hata mwaka unamaliza, lakini hawa wana wasiwasi pia. Waombeeni pia wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala kwa sababu kazi hizi ni ngumu, hujui kesho itakuaje,” amesema  Rais Magufuli.