Magufuli ahoji utendaji kazi wa viongozi Dar

Muktasari:

Rais John Magufuli amehoji hatua viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam kushindwa kusimamia ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema mambo ya hovyo  yanayofanyika katika mkoa wa Dar es Salaam yanamfanya ajiulize kama mkoa huo kuna viongozi.

Magufuli amesema hayo leo Jumapili Septemba 22, 2019 wakati akiwaapisha Ikulu jijini Dar es Salaam viongozi mbalimbali aliowateua Ijumaa iliyopita ya Septemba 20,2019.

Miongoni mwa miradi ambayo Rais Magufuli ameonyesha kutoridhishwa nayo ni ya uboreshaji wa ufukwe wa Coco uliopo Manispaa ya Kinondoni.

Meya wa Manispaa hiyo ni Benjamin Sitta na mkuu wa wilaya hiyo ni Daniel Chongolo huku mkoa huo ukiongozwa na Paul Makonda.

Magufuli amehoji kitendo cha Meya wa Manispaa hiyo kumkabidhi mkandarasi mradi huo wa Coco ambao unaingiliana na ujenzi wa barabara inayopita baharini ya Salender.

Mkuu huyo wa nchi aliwachambua viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wakati akijenga hoja kuhusu viongozi wa mkoa wa Morogoro walioshindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo na kuwataka viongozi wenye dhamana kuwatumikia wananchi wanaowaongoza.

Amesema Dar es Salaam yanafanyika mambo ya hovyo, huwezi kuamini  kama kuna viongozi, “Ni mambo ya ajabu, wewe waziri ukakabidhi site (eneo) au meya wapi na wapi? ni mambo ya ajabu. Lakini site iliyokabidhi kwa Sh14 bilioni ina maswali mengi ya kujiuliza.”

Amesema mkandarasi aliyekabidhiwa ndiye alishindwa katika soko la Mwanjelwa mkoani Mbeya ana mradi mwingine haujakamilika lakini amepewa kazi ya Coco Beach.

Septemba 19, 2019 mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alitangaza kuufunga ufukwe huo kwa muda miezi sita ili kupisha uboreshaji wa eneo hilo huku akisema kampuni ya Tanzania Bulding Works ndio itakayotekeleza.

Kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli ameeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, huwezi ukajenga muundo mkubwa ndani ya mita 60 kutoka baharini au ziwani, lakini chakushangazwa alipokabidhiwa kuna mradi mwingine wa ujenzi wa daraja la Salender.

“Mradi huu wa Salender una barabara nne kuna nyingine inatoka Hospitali ya Aga Khan inapita katika daraja inakwenda hadi Coco Beach. Kibao kipo sasa unajiuliza miradi yote ni ya Serikali, huu mradi ,mkubwa tulitoa Sh200bilioni utapita wapi? amehoji.

“Je watajenga muundo wa hoteli pale, je wale wachuuzi watafukuzwa. Mradi wowote ambao ni positive kwa watu lazima uwatafutie njia mbadala, lazima uwapeleke mahali ili mradi ukikamilika warudi,” amehoji.

Amesema Coco Beach haiwezi kujengwa kwa Sh14 bilioni, wakati kinachotakiwa ni kutengeneza njia sanjari na  kuweka vitu vya kukalia  kuwapa fursa ya watu wanaotaka ufukweni, kumpumzika.

“Unajenga muundo wa nini ? why 14 bilion? Kwa nini,” amehoji Rais Magufuli.