Magufuli aibua mapya ya Lugola

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema hajui kwa nini kila Waziri wa Mambo ya Ndani anayemteua kwenye awamu yake ya utawala hulazimika kutengua uteuzi wake huku akimtaka George Simbachawene kuitendea haki wizara hiyo.

Ametoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kumwapisha Simbachawene aliyemteua wiki iliyopita kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kuchukua nafasi ya Kangi Lugola aliyetengua uteuzi wake.

Mbali na Simbachawene, Rais Magufuli alimwapisha Azzan Zungu kuwa Waziri wa Muungano na Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais na mabalozi watatu ambao ni; Maimuna Tarishi (Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Geneva, Uswisi), Hussein Kattanga (Balozi wa Tanzania Tokyo, Japan) na Profesa Kennedy Gastorn kuwa Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa (UN), New York, Marekani.

Baada ya kumaliza kuwaapisha na hotuba fupi za mawaziri hao wapya na ile ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi uliwadia wasaa wa Rais Magufuli kuzungumza.

Hotuba ya Rais Magufuli ambayo haikuzidi dakika 15, aliitumia zaidi kutoa maagizo na maelekezo kwa Simbachawene huku akigusia jinsi mtangulizi wake kwenye wizara hiyo (Lugola), alivyoshindwa kuitendea haki.

Rais Magufuli alisema kuna namna ya kuongoza wizara hiyo huku akitolea mfano, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amedumu kwenye wizara hiyo tangu alipomteua mara ya kwanza Desemba 10, 2015.

Hali hiyo ni tofauti na Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ndani ya kipindi chake cha uongozi hadi sasa, Simbachawene amekuwa waziri wa nne akitanguliwa na Charles Kitwanga, Dk Mwigulu Nchemba na Kangi Lugola.

Alimsifu Simbachawene kwa hotuba nzuri aliyoitoa akisema, “umezungumza vizuri hapa, kwamba wewe (Simbachawene) huna nyota hata moja, hivi vyombo vya ulinzi na usalama vina namna yake ya kuviongoza.”

“Ndiyo maana Waziri Mwinyi amekaa sana Wizara ya Ulinzi, hawezi kusimama pale mbele na kuwatukana mabrigedia hawa, anajua jinsi ya kufanya nao kazi, katumie mbinu hizo hizo,” alisema Rais Magufuli

Awali, kwenye hotuba yake, Simbachawene alisema ataviheshimu vyombo vya usalama vifanye kazi yake huku yeye akishughulika na mambo ya utawala.

“Umenipa jukumu nikusaidie katika kusimamia vyombo hivi ambavyo kwa sehemu vinafanya kazi ya ulinzi na usalama na ninatambua mimi si amiri jeshi mkuu.

Rais Magufuli aliongeza; “Ndiyo maana mnaona wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wana uwezo wa kuripoti moja kwa moja kwa Rais, sasa ukishapima hayo, hii inaweza kukusaidia sana jinsi ya kuongoza.”

“Najua wewe ni mwanasheria, ulipoanza hapa kuzungumza nikamwona IGP (Simon Sirro) anatingisha kichwa, nafikiri amefurahi sana,” alisema Rais Magufuli huku IGP Sirro akisimama akiwa na uso wa tabasamu na kupiga saluti ya utii kwa Amiri Jeshi Mkuu huyo wa nchi.

“Saa nyingine alikuwa anakuja kwangu (IGP) analalamika anasema nimeshaambiwa hawa niwatoe, lakini amri haizungumzi hivyo, nikamwambia bwana nenda kawatoe, lakini kiukweli saa nyingine siyo utaratibu na mara nyingi tukifuata utaratibu itatusaidia,” alisema Rais Magufuli

Ingawa Rais Magufuli hakumtaja kwa jina Lugola, lakini alifahamika kwa kuadhibu, kurekebisha, kushusha vyeo na kuwajibisha wakosefu huku mara kadhaa akitoa maagizo kwa IGP Sirro ya kuhamisha makamanda wa polisi.

Januari 22, mwaka jana, IGP Sirro alitekeleza agizo alilopewa na Lugola la kuwahamishia makao makuu ma - RPC watatu kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili alizoziibua Lugola.

Makamanda hao ni Ramadhan Ng’azi (Arusha), Salum Hamduni (Ilala) na Emmanuel Lukule (Temeke).

Katika kipindi cha siku 571 cha Lugola kukaa ndani ya wizara hiyo kuanzia Julai Mosi, 2018 hadi Januari 23 alipotenguliwa, alifanya ziara mbalimbali mikoani na kuendesha vikao kazi vya taasisi zilizo chini yake na alishuhudiwa akiwafukuza vikaoni makamanda wa polisi, kuagiza washushwe vyeo, wengine kuwekwa mahabusu na kuhamishwa.

Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Lugola na kukubali kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali, John Kingu na kumng’oa Mkuu wa Jeshi la Zimamoto, Kamishna Thobias Andengenye.

Uamuzi huo aliuchukua wakati akipokea nyumba za askari Magereza Ukonga, Dar es Salaam baada ya kuelezea mkataba aliouita mbovu uliojaa ufisadi wa thamani ya Sh1 trilioni, ambao ulikiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma na kutofuata taratibu za mikataba ya umma uliofanywa na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji.

Rais Magufuli alisema Andengeye alisaini mkataba huo ambao haujapangwa kwenye bajeti na haujapitishwa na Bunge ambao ulilenga kununua vifaa mbalimbali vya zima moto zikiwamo ‘drones.’

Rais Magufuli alisema wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wote wa Tanzania waliokuwa wanakwenda katika majadiliano walikuwa wanalipwa Dola 800 za posho ya vikao na tiketi za ndege.

Kuna nini wizarani?

Rais Magufuli alimwambia Simbachawene, “nakupeleka katika wizara ngumu’ na ugumu huo unaweza kuusababisha wewe au ugumu unaweza kuurahisisha wewe, narudia kusema Wizara ya Mambo ya Ndani imehusika kwenye tuhuma nyingi.”

“Wamekuwa wakiambiwa warekebishe, mawaziri wengi wamekuwa wakiambiwa, sifahamu kuna mdudu gani pale, nimeamua kukupeleka wewe, sijui Mgogo, sijui Mhehe nenda kayasimamie,” alisema Rais Magufuli huku akimkabidhi nyaraka za madudu ya wizara hiyo na akimtaka akaanze nazo huku akimpa tahadhari juu ya watendaji wa wizara hiyo.

“Naibu waziri (mambo ya ndani- Hamad Masauni) anajua, ingawaje hakuhusishwa sana alikuwa anapewa nakala ya madokezo ananyamaza, angeweza akaja hata mapema serikalini akaeleza ninaona dokezo limetolewa na waziri wangu (Lugola) linahusu hiki. Sifahamu kwa nini alitulia,” alisema Rais Magufuli huku Masauni aliyekuwapo akisimama na kuinama kwa heshima.

“Naibu katibu mkuu amehusika sana, tangu kuanza kwake mpaka mwisho, kuna watendaji wengine kwenye jeshi la zima moto wamehusika, ndiyo hao wengine walikuwa wanakwenda kwenye vikao wanapewa dola 500, dola 300 na wanapewa Laptop,” aliongeza.

Ingawa Rais Magufuli hakumtaja kwa jina naibu katibu mkuu huyo lakini wizara ya mambo ya ndani ina naibu katibu mkuu mmoja ambaye ni Ramadhan Kailima. Kailima aliteuliwa na Rais Magufuli kushika wadhifa huo akitoka kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Waziri aliyetumbuliwa (Lugola) analeta kibarua anasema nithibitishe tu, nathibitishaje kitu ambacho sikijui, unakwenda wizara sijui ina mapepo, nenda kasimamie na yale utakayoweza kubadili kayabadili na wanaoweza kuondolewa kawaondoe,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alieleza katika mkataba huo ulihusisha kukopa fedha benki za nje pasipo kuonyesha itakuwa na riba kiasi gani, “Tumewaachia watu wa Takukuru, sifahamu kama watafanya kazi vizuri au wataogopa, naamini watafanya kazi bila kujali nafasi za watu.”

Alichokisema Zungu

Awali, Zungu alisema ataanza na suala la marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kwani siku za hivi karibuni imeanza kurejea sokoni.

Zungu alisema wizara aliyopewa ni ngumu na ina changamoto nyingi.