VIDEO: Magufuli aikabidhi Takukuru ripoti ya miradi 107 yenye dosari

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli ameikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)   ripoti iliyobainisha dosari katika miradi ya maendeleo 107 iliyotembelewa wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.

Dar es Salaam. Rais  wa Tanzania, John Magufuli amemkabidhi naibu mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo ripoti ya miradi 107 iliyobainika kuwa na dosari.

Miradi hiyo ilibainika kuwa na kasoro ilipotembelewa kwa ajili ya kuzinduliwa na kukaguliwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru zilizofikia kilele chake leo Jumatatu Oktoba 14, 2019.

Rais Magufuli amekabidhi ripoti hiyo leo katika maadhimisho ya kilele hicho na kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere yaliyofanyika mkoani Lindi.

Awali, kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Mzee Mkongea Ally alimkabidhi Rais Magufuli ripoti ya miradi ya Sh90.28 bilioni iliyokutwa na dosari.

“Sogea hapa mbele nikukabidhi ripoti hii, zege halilali. Naikabidhi hii ripoti ukafanye ukaguzi kila ukurasa, kila nukta na ukachambue wale wote wanaohusika kupelekwa mahakamani. Usisite wapeleke mahakamani,” amesema Rais Magufuli wakati akimkabidhi Brigedia  Jenerali Mbungo ripoti hiyo.

Rais Magufuli amesema viongozi wakubwa watakaobainika kuhusika kuhujumu miradi kwenye ripoti hiyo, majina yao yapelekwe kwake ili naye aweze kuifanyia kazi.

 “Nataka Tanzania inyooke hatuwezi tukawa tunapeleka fedha inachezewa tu, na ndio maana nawapongeza sana vijana hawa wakukimbiza Mwenge,” amesisitiza Rais Magufuli.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ameeleza kuwa tathmini ya miradi iliyofanyika katika mbio hizo imekwenda vizuri.

“Ni matumaini yangu kwamba ofisi ya Waziri Mkuu pia itafuatilia miradi hii maana najua na Waziri Mkuu huwa anafuatilia hadi nukta,” amesema kiongozi huyo.

Katika risala yake,  Mkongea Ally amesema katika maeneo walikopita  mbali na wananchi kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo, wamemuomba kufuatilia kwa ukaribu miradi ya maji na kuwachukulia hatua stahiki wanaobainika kuhujumu miradi hiyo.