Magufuli aionya CCM kuhusu upinzani

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli akifungua kikao cha Viongozi wa Mikoa na Wilaya, Watendaji wa Chama na Jumuiya zake wa kilichofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam jana. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Wakati joto la uchaguzi mkuu kwa mwaka huu likianza, Rais John Magufuli amewataka viongozi wa CCM wasibweteke na uimara wa chama hicho, akisema wapinzani nao wamebadilika na sasa wana mikakati mingi ya kutaka kushinda.

Mwenyekiti huyo wa chama hicho tawala alitoa onyo hilo katika mkutano wa viongozi wa chama hicho wa ngazi zote uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliohusisha wenyeviti na makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya zote nchini, ulilenga kusalimiana na kushirikisha viongozi hao kuhusu serikali yao.

Amesema hayo ikiwa takriban miaka minne baada ya mchuano mkali uliojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2015 ulioshuhudia wapinzani wakiungana na kufanikiwa kupata idadi kubwa ya kura za urais, huku wakiingiza idadi ya wabunge iliyoweka rekodi tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.

Katika uchaguzi huo, Magufuli alipata kura milioni 8.8 huku mgombea wa upinzani, Edward Lowassa, aliyeungwa mkono na vyama vinne, akipata kura milioni 6.07.

“Lazima sisi kama chama tujitathmini,” alisema Rais Magufuli, ambaye pia ameahidi uchaguzi ujao kuwa wa amani, huru na wa haki.

“Tuwe na maandalizi ya uhakika katika uchaguzi. Ni lazima tufanye hivyo kwa sababu kuna mabadiliko mengi.

“CCM ya leo si kama ya nyuma. Lakini tutambue kwamba washindani wetu wa leo si sawa na wa nyuma. Nao wanabadilika, wanabuni mikakati mingi ya wazi na ya ndani, tusibweteke.”

Na ingawa CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 90 katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, Rais alisema ushindi huo usiwafanye wabweteke.

Hata hivyo, vyama kadhaa vya upinzani, vikiwemo vya Chadema, ACT Wazalendo na NCCR-Mageuzi vilisusia uchaguzi huo kwa madai ya wagombea wao kutotendewa haki na hivyo wagombea wa CCM kutangazwa washindi bila kupigiwa kura kutokana na kukosa wapinzani.

Lakini alikuwa na neno la faraja kwa viongozi hao wa wilaya na mikoa.

“Licha ya wao (wapinzani) kujipanga, ukitazama kwa umakini, Tanzania kwa sasa haina vyama vya upinzani vilivyo imara sana vinavyoweza kushindana na CCM,” alisema Magufuli.

“Unapoona watu wengi wanahama huko wanakuja CCM, ujue chama kina mvuto. Chama kiko imara. Tusibabaishwe na kelele ndogondogo za washindani wetu ambao nguvu zao zimekwisha.”

‘Hakuna mazingira sawa’

Lakini wapinzani walipokea kauli ya Rais kuwa nguvu za “washindani wao zimekwisha” kwa maoni tofauti, huku mjumbe wa Kamati Kuu ya CUF, Abdul Kambaya akisema “hakuna mazingira sawa ya ushindani katika uchaguzi”.

“Wakati tunaingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, wapinzani hatukupewa nafasi ya kurudisha fomu. Sasa unawezaje kupima nguvu yetu? Nadhani kwa kuwa alikuwa akiongea na viongozi wa CCM, alitaka kuwajengea ari ya kujiamini, wawe na morali wa uchaguzi,” alisema Kambaya.

Naye mkurugenzi wa mawasiliano wa Chadema, John Mrema alikosoa kikao hicho akisema kinaonyesha hofu ya chama dhidi ya upinzani kwa sababu hakipo katika chama hicho.

Hata hivyo, Mrema alisema anashangaa mwenyekiti wa CCM kukiri kwamba upinzani una mikakati mingi ya wazi. Alisema jambo hilo ndiyo linalomtia hofu na kuudhibiti upinzani wakati wa uchaguzi na wakati wote.

“Kama wanadhani upinzani ni dhaifu, kwa nini wasiweke Tume huru ya uchaguzi, tuingie uwanjani tushindane kwa haki? Hicho kitu hawataki kwa sababu wanajua nguvu yetu,” alisema Mrema.

Uchaguzi mkuu, ambao huhusisha uchaguzi wa Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani, unatarajiwa kufanyika wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba na Rais Magufuli alikuwa na neno kwa viongozi hao wa CCM.

“Wakati wa mchakato wa uchaguzi, tusiende na majina mfukoni; kwamba huyu ni wa mwenyekiti, huyu ni wa katibu,” alisema mwenyekiti huyo wa CCM.

“Wakati mwingine unakuta mwenyekiti na katibu wanagombana. Tuweke maslahi ya chama chetu mbele.

“CCM ina misingi, kanuni na taratibu za kupitisha majina ya wagombea wanaofaa, lakini baadhi ya viongozi hawaifuati.”

Alisema tabia hiyo imefanya chama kuwa kinapoteza wagombea wazuri kwa sababu ya migogoro ya ndani licha ya kuwa na wanachama wazuri ambao hunyimwa fursa ya kugombea kwa sababu tu viongozi wana watu wao.

Awapa majukumu viongozi

Rais Magufuli aliwakumbusha viongozi hao wajibu wao wanapokuwa maeneo ya kazi, akiwapa majukumu matatu ambayo ni kuisimamia Serikali katika maeneo yao, kukijenga chama kwenye ngazi ya mashina na matawi pamoja na kuitetea Serikali na kutangaza mafanikio yaliyopatikana.

Alisema miradi mingi ya Serikali inafanyika wilayani na mikoani, hivyo, aliwataka viongozi hao kufuatilia utekelezaji katika maeneo yao na wakiona haiendi vizuri, watoe taarifa kwa katibu mkuu.

Aliwataka viongozi hao kutangaza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa mambo mengi makubwa yamefanyika, hivyo, ni wajibu wao kuwaeleza wananchi.

“Nitashangaa kama kuna kiongozi wa CCM ambaye hatambui mageuzi makubwa yaliyofanyika katika awamu hii.

“Tumejenga hospitali 69 za wilaya, huduma za umeme mpaka vijijini, ujenzi wa reli ya kisasa kwa takribani Sh7 trilioni, mradi wa kufua umeme wa Stiglers. Mambo ni mengi,” alisema Rais Magufuli.

Pia, Rais Magufuli aliwataka viongozi hao kukiimarisha chama kwenye ngazi ya mashina na matawi kwa sababu nguvu ya chama inaanzia huko. Aliwataka kuongeza nguvu katika kuimarisha mashina na matawi katika maeneo yao.

Wajumbe 1,780 wahudhuria

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi 1,780 huku wajumbe 20 wakishindwa kuhudhuria.

“Ndugu mwenyekiti, ulinipa maelekezo ya kuitisha mkutano huu na ndani ya siku saba, wajumbe 1,780 wamehudhuria kati ya wajumbe 1800 waliotakiwa kuwepo,” alisema Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Wakati huohuo, Dk Bashiru amesema CCM iko kwenye mchakato wa kuandaa ilani ya uchaguzi na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula ataongoza kamati hiyo huku Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwa makamu mwenyekiti na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa mjumbe.