Magufuli akerwa ushuru, azionya halmashauri

Muktasari:

Rais John Magufuli ametoa onyo kwa wakurugenzi na watendaji wa halmashauri kuacha kuwatoza ushuru wafanyabiashara wanaosafirisha mazao yasiyozidi tani moja na wafanyabiashara wenye mitaji isiyozidi Sh4 milioni kwa mwaka  ambao wana vitambulisho.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema ni marufuku kwa wakurugenzi na watendaji wa halmashauri kuwatoza ushuru wasafirishaji wa mazao chini ya tani moja na wafanyabiashara wadogo wenye vitambulisho vya wajasiriamali.

Ametoa onyo hilo hiyo leo Jumanne Aprili 30 katika viwanja vya Mwakangale wilayani Kyela katika ziara yake ya siku nane mkoani Mbeya.

Amesema wapo watendaji wa halmashauri wanaoendelea kutoza ushuru kwa wafanyabiashara hao kwa kudhani kuwa wanapoacha wanapunguza mapato.

“Narudia kwa wakurugenzi na watendaji wote wa halmashauri msiwatoze wananchi ushuru wa mzigo wowote usiozidi tani moja. Mkulima wewe safirisha kutoka hapa peleka mahala popote hakuna wa kukutoza ushuru, na hii sheria imepitishwa na Bunge hayupo yeyote wa kuitengua kwa hivyo mkurugenzi ukitengua umevunja sheria una wajibu wa kufukuzwa kazi.”

“Tuzingatie sheria ya kuwalinda wakulima, pakia viazi, maharage, njugu, chochote ilimradi kisizidi tani moja hakuna kulipia, ukizidisha mie simo,” amesema Rais  Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli akizungumzia vitambulisho vinayotolewa kwa wafanyabishara wadogo wenye mtaji wa chini ya Sh4milioni, alisema  hatua ya kutoa vitambulisho hivyo inawaumiza watendaji kwa kuwa huko nyumba walizoea kula.

“Wapo wanaouza uji, mahindi sokoni, mchicha, maandazi, vitumbua mtaji wake hauwezi kufika Sh 4 milioni kwa mwaka, ukishakuwa na kitambulisho chako unalipia Sh20,000 kwa mwaka mzima utafanya bishara popote ilimradi hauvunji sheria hakuna wa kukubughudhi, viongozi madiwani mtoe  ufafanuzi kwa wananchi hawa wafaidike na matunda ya kuwa Watanzania,” amesema Rais Magufuli.