Magufuli akunwa na Balozi wa Ufaransa, aagiza apewe vitabu vya Kiswahili

Monday September 16 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi, [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameigiza Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kumpa vitabu vya Kiswahili na kamusi Balozi wa Ufaransa nchini humo, Frederick Clavier kama zawadi kutokana na kuzungumza vyema lugha hiyo.

Ametoa agizo hilo leo Jumatatu Septemba 16, 2019 wakati wa hafla ya uzinduzi wa rada mbili za kuongezea ndege katika uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na ule wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) huku akimshukuru Balozi Clavier na kumuombea kwa Mungu amjalie kwa kukienzi Kiswahili.

Rais Magufuli amemsifu na kumshukuru Balozi Clavier kwa kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha  wakati akiwasilisha hotuba yake katika hafla hiyo akisema hiyo ndio faida kujua lugha hiyo ya Taifa.

“Huyu Baba ametoka Ufaransa maelfu ya kilomita, amefika hapa hivi karibuni anazungumza Kiswahili vizuri tu. Unafikiri akimtafuta mwanamke atamkataa kwa Kiswahili kizuri cha namna hii,” amehoji  Rais Magufuli huku akiibushwa vicheko kwa umati wa watu uliojitokeza

“Lakini utamkuta mtu wa hapa hapa wa bongo anajifanya Kiingereza ndio chake ni kupungukiwa. Huyu Mfaransa (Clavier) wala hajazaliwa Tanzania lakini anapiga Kiswahili kizuri, lakini wengine tunafikiri kuzungumza Kiingereza ndio kujua,” amesema

Amefafanua Balozi Claveir amezungumza kwa unyenyekevu mkubwa lugha ya Kiswahili ambayo ni ya 10 duniani kwa kuzungumzwa na alitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kukipenda kilicho chao.

Advertisement

Awali, akiwasilisha hotuba yake, Balozi Clavier amesema kwa niaba ya nchi hiyo amemshukuru  Rais Magufuli kwa kuhudhuria uzinduzi huo, akisema Ufaransa inaunga mkono juhudi za kuimarisha uchumi wa viwanda utakaosaidia kufikisha Taifa kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Mradi wa huo wa rada umetekeleza na mkandarasi, Thales Air Sytem (SAS) kutoka Ufaransa na rada mbili zikatumika kuongozea ndege kwenye viwanja vya JNIA na KIA umekamilika huku zingine zikiwa kwenye mchakato.

Advertisement