Magufuli amjulia hali Askofu Mkuu Ruwa’ichi, aifariji familia ya CDF Mabeyo

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli akisalimiana kwa furaha na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi ambaye anapatiwa matibabu katika Taasisi hiyo ya Mifupa Muhimbili  (MOI) mara baada ya kufanyiwa upasuaji wa Kichwa 

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli amemjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi anayepatiwa matibabu Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).

-Pia, amekwenda Msasaji jijini Dar es Salaam kumpa pole Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (JWTZ) Jenerali Venance Mabeyo ambaye amefiwa na mwanae Nelson Mabeyo katika ajali ya ndege.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli leo Jumatatu Septemba 23, 2019 amemjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi anayepatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais Magufuli amemkuta Askofu Mkuu Ruwa’ichi akiwa anaendelea vizuri tofauti na hali ilivyokuwa alipomtembelea Septemba 10, 2019 siku aliyoletwa MOI akitokea Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro alikougua ghafla baada ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi.

Akiwa MOI, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amefanyiwa upasuaji na timu ya madaktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa mafanikio na sasa anaendelea vizuri.

Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa kwake na kuimarika kwa hali ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi na amewapongeza madaktari bingwa wa MOI kwa kumtibu kwa mafanikio makubwa.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi, Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Padre, Alister Makubi wamesali sala ya pamoja ya kumshukuru Mungu kwa uponyaji na kuwaombea wagonjwa wote wapone haraka.

Baada ya kutoka MOI, Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akiwemo Baba Mzazi wa Daktari wa Rais, Mzee Wilson Ngwale aliyelazwa hospitalini hapo.

Kabla ya kutembelea wagonjwa, Rais Magufuli amekwenda Msasani Jijini Dar es Salaam kumpa pole Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (JWTZ) Jenerali Venance Mabeyo ambaye amefiwa na mwanae Nelson Mabeyo (aliyekuwa Rubani) ambaye amefariki dunia leo asubuhi baada ya ndege aliyokuwa akiiendesha kupata ajali muda mfupi baada ya kuruka kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Seronera Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Mapema leo asubuhi, Rais Magufuli ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.