Magufuli amjulia hali Askofu Ruwa’ichi

Muktasari:

  • Rais John Magufuli leo Jumanne Septemba 10, 2019 amemjulia hali Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,  Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi ambaye amelazwa taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI), jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Rais John Magufuli leo Jumanne Septemba 10, 2019 amemjulia haliAskofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,  Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi ambaye amelazwa taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI), jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa leo inaeleza kuwa Askofu Ruwa’ichi alipata ugonjwa wa kiharusi juzi mkoani Kilimanjaro na alipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Kilimanjaro (KCMC) na baadaye kuhamishiwa Moi alikofanyiwa upasuaji wa kichwa.

Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu wa Moi, Profesa Joseph Kahamba amesema baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali ya Ruwa’ichi imeanza kuimarika.

Magufuli pamoja na madaktari na wauguzi wa Moi wamemuombea Ruwa’ichi  apone haraka na kuendelea na majukumu yake ya kila siku.

Akiwa katika wodi hiyo ya wagonjwa mahututi, Magufuli amewajulia hali wagonjwa wengine waliofanyiwa upasuaji wa kichwa na kuelezea kufurahishwa na maendeleo makubwa yaliyopatikana katika taasisi hiyo ambayo sasa inatoa matibabu ya upasuaji mkubwa ambayo hayakuwa yanapatikana nchini.

Profesa Kahamba amemshukuru Magufuli kwa Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika taasisi hiyo ikiwemo kukamilisha jengo, kuongeza vitanda katika vyumba vya upasuaji na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Magufuli amewapongeza madaktari na wauguzi wa Moi kwa kazi kubwa wanayoifanya na ameahidi kutoa Sh1.5 bilioni kwa taasisi hiyo kwa ajili ya kununulia vipandikizi vya  wagonjwa wanaopatiwa matibabu baada ya kuvunjika.

Mkurugenzi mtendaji wa Moi, Dk Respecious Boniface amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fedha hizo na kumhakikisha kuwa zitasaidia matibabu ya Watanzania wengi.

Akiwa njiani kurejea Ikulu, Magufuli ametembelea kituo cha Polisi cha Selander Bridge na kuzungumza na askari wa kituo hicho, kuagiza WP 4160 Beatrice Mlanzi kupandishwa cheo kutoka Koplo na kuwa Sajenti baada ya kuonesha utimilifu katika kazi.