VIDEO: Magufuli ampa jukumu la kwanza Majaliwa

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuangalia namna atakavyofanya kuhakikisha mifuko iliyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa kawaida inakuwa na tija.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuangalia namna atakavyofanya kuhakikisha mifuko iliyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa kawaida inakuwa na tija.

Amesema katika jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi ni lazima waifahamu mifuko hiyo na programu zote zinazotolewa na Serikali kwa ajili yao.

“Nakuagiza waziri mkuu hii ikawe kazi yako ya kwanza kushughulikia. Ikiwezekana muangalie  uwezekano wa kuiunganisha ili ifanye kazi kwa tija na kupunguza gharama za uendeshaji. Mifuko hii inapaswa kuwa na tija kwa wananchi wa kawaida wakiwemo wamachinga, mama lishe na wajasiriamali,” amesema Magufuli.

Magufuli ameeleza hayo leo Ijumaa Novemba 13, 2020 katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la 12, jijini Dodoma.

Baadhi ya mifuko hiyo ni mfuko wa maendeleo ya vijana, mfuko wa maendeleo ya wanawake, mfuko wa taifa wa kuendeleza wajasiriamali, mfuko wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na mfuko wa kilimo kwanza.

Magufuli aliyechaguliwa kuwa rais kwa awamu ya pili amesema Serikali itaendelea kutekeleza programu za kukuza ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa ndani na nje ya nchi.