Magufuli amtumia Slaa kuikomboa Karatu

Muktasari:

Jimbo la Karatu ndilo lililomuibua Dk Slaa, ambaye alipata umaarufu nchini kutokana na kupinga ufisadi na kuuanika, ikiwemo kutangaza orodha ya mafisadi, maarufu kama List of Shame.

Karatu. Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, John Magufuli jana alimtumia Balozi Wilbroad Slaa kama turufu ya ushindi katika jimbo la Karatu ambalo limekuwa chini himaya ya upinzani kwa miaka 25.

Jimbo la Karatu ndilo lililomuibua Dk Slaa, ambaye alipata umaarufu nchini kutokana na kupinga ufisadi na kuuanika, ikiwemo kutangaza orodha ya mafisadi, maarufu kama List of Shame.

Ametumia silaha hiyo siku moja baada ya kuwapandisha jukwaani wanasiasa wawili maarufu mkoani Arusha, Edward Lowassa na Abdulrahman Kinana wakati akimnadi mgombeas wa CCM wa Arusha Mjini, jimbo ambalo limeshikiliwa na upinzani tangu mwaka 2010.

Magufuli jana alikuwa anaendelea na kampeni zake katika mkoa wa Arusha, ambapo mapema asubuhi alizungumza na wananchi wa Monduli mjini Makuyuni, na aliomba kura zake na za mgombea wa jimbo hilo, Fred Lowassa.

Tangu Alhamisi, Magufuli amekuwa Arusha akiomba kura na kuwapigia debe wagombea ubunge wa CCM, ambao ni pamoja na Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Noah Lebrus Molel (Arumeru Magharibi), John Pallangyo (Arumeru Mashariki), Stephen Kirusya (Longido) na William Ole Nasha (Ngorongoro).

Baada ya mkutano wa Makuyuni, Magufuli alikwenda mjini Karatu jana mchana na kuhutubia umati mkubwa wa wananchi wa uliofurika katika Uwanja wa Mnadani, ambako alimnadi Daniel Awaki.

“Mambo mawili yamenileta Karatu,” alisema Magufuli.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kumtambua na kumheshimu Dk Slaa kama kiongozi mzalendo, mpambanaji kwa mchango wake katika maendeleo ya watu wa Karatu na taifa la Tanzania.

Pia alisema jambo la pili ni kumpigia debe Awaki na pia kuwaeleza wananchi wa Karatu ukweli kuhusu haja ya wao kuachana na wagombea wa upinzani na kuwapigia kura wa CCM.

Tangu uchaguzi wa vyama ulipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1995 baada ya siasa za ushindani kurejeshwa mwaka 1992, jimbo la Karatu limekuwa na wabunge kutoka vyama vya upinzani.

Jingine ambalo halijawahi kuangukia CCM ni Moshi Mjini.

Magufuli alikumbushia historia ya jimbo hilo kwenda upinzani, akisema ilitokana na Dk Slaa kukatwa katika mchakato baada ya kushinda kura za maoni ndani ya CCM mwaka 1995.

Badala yake, CCM ilimuweka Patrick Qorro kugombea Karatu, huku Dk Slaa akijitoa na kujiunga na Chadema na kushinda ubunge na pia kushinda tena mwaka 2000 na 2005 lakini mwaka 2010 alijitosa kuwania urais.

Magufuli alisema Dk Slaa alikuwa mbunge mahiri na alipigania maendeleo ya Karatu na kukumbusha wakati akiwa Waziri wa Ujenzi alikuwa anamuomba kushughulikia miradi ya barabara na kwamba mafanikio yake ni kujengwa kwa barabara ya lami kutoka Makuyuni hadi Karatu licha ya upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wa mazingira waliokuwa wanadai barabara hiyo inapita mbuga ya Manyara.

Pia alisema katika viongozi wa upinzani waliowahi kujitokeza nchini, anamuweka Slaa kuwa wa kwanza kutokana na kazi kubwa aliyofanya Karatu na umahiri wake wa kujenga hoja.

“Slaa alikuwa mtu makini, mahiri wa kujenga hoja na alikuwa anawawakilisha vizuri wananchi wa Karatu bungeni. Na ndugu zangu ninapenda kuwaambia kuwa watu wa upinzani si wabaya ndio maana safari hii niliwateua Profesa Kitila Mkumbo na Anna Mghwira waliokuwa upinzani pia,” alisema Magufuli.

Dk Slaa alijitoa Chadema mwaka 2015, akisema hakukubaliana na kutofurahishwa na hali ya mambo katika chama hicho na hasa kitendo cha kumpitisha Edward Lowassa kama mgombea urais.

Baada ya kujitoa Chadema, Magufuli aliposhinda urais 2015, alimteua Dk Slaa kuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden na pia anaiwakilisha Tanzania katika nchi nane nyingine za Ulaya ambazo ni Denmark, Finland, Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine.

Hata baada ya kuondoka kwa Dk Slaa, bado Karatu iliendelea kuchagua wabunge kutoka Chadema. Mchungaji Israel Natse alikuwa mbunge kuanzia 2010 hadi 2015 na kufuatiwa na William Qambalo, ambaye amemaliza muda wake.

Magufuli amewaahidi watu wa Karatu kuwa wakimchagua Aweki, watamrahisishia kazi na kushughulikia changamoto zao.