Magufuli aonya tabia ya kupandisha bei ya bidhaa mfungo wa Ramadhan

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka watu wenye tabia za kupandisha bei ya vitu katika mfungo wa Ramadhan kuacha mara moja tabia hiyo pia amewataka watu wa madhehebu mengine kushirikiana na waislamu katika mfungo huu

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema anafahamu uwepo wa watu wenye tamaa ya kupandisha bei katika kipindi cha mfungo wa Ramadhan hivyo amewataka kuacha tabia hiyo mara moja.

Ameyasema hayo leo Jumapili ya Mei 19, 2019 katika Mashindano ya 20 ya kusoma na kuhifadhi Quran  Afrika yaliyofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Amesema kufanya hivyo ni dhambi mbele ya mwenyezi Mungua kufanya hivyo hakuwezi kumtajirisha mtu hasa kwa kupandisha bei ya vile vitu vinavyotumika sana katika mfungo huu.

“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa Mamlaka husika za serikali kufuatilia suala hili kwa ukaribu sana.” Amesema Magufuli

Mbali na hilo amewataka watu wa madhehebu mengine na wale wasiokuwa na dini kuendelea kushirikiana na Waislamu katika kutimiza mfungo wa mwezi huu ambao ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu.

“namuomba Mungu awalipe malipo stahiki juu ya kile mnachokifanya katika funga zenu, Mimi mwenyewe sijafunga lakini siku ya kufumgua waislamu ntakua nanyi katika pilau.” Amesema Magufuli.