VIDEO: Magufuli aonya viongozi kupitisha wagombea wao uchaguzi 2020

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Rais John Magufuli amewataka viongozi wa mikoa wa chama hicho kutokuwa na majina yao mfukoni katika  mchakato wa kura maoni kuwapata wagombea wa udiwani na ubunge.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania, Rais John Magufuli amewataka viongozi wa mikoa wa chama hicho kutokuwa na majina yao mfukoni katika  mchakato wa kura maoni kuwapata wagombea wa udiwani na ubunge.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 24, 2020  jijini Dar es Salaam alipokutana na viongozi wa mikoa, wilaya na jumuiya za chama hicho kutoka mikoa yote nchini.

Amewataka viongozi hao kuweka mbele maslahi ya chama hicho kwa kuchagua wagombea wenye sifa na wanaokubalika kwa wananchi.

Amesema ndani ya CCM, kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

"Wakati wa mchakato wa uchaguzi, tusiende na majina mfukoni, kwamba huyu ni wa mwenyekiti, huyu ni wa katibu. Wakati mwingine unakuta mwenyekiti na katibu mkuu wanagombana. Tuweke maslahi ya chama chetu mbele," amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema chama hicho kiko imara, viongozi  wasibabaishwe na kelele ndogo  za washindani wao ambao nguvu zao zimekwisha.

"Tuache kugombana hasa kwenye nafasi za ubunge na udiwani. Wakati mwingine tunawapoteza wagombea wazuri mpaka wanahama, mambo haya hayatatokea tena," amesema mwenyekiti huyo wa CCM.