VIDEO: Magufuli aruhusu makontena yenye mchanga wa madini kuuzwa

Muktasari:

Rais wa Tanzania John Magufuli ameruhusu makontena yenye mchanga wa madini ya dhahabu kuuzwa, akibainisha kuwa tayari mteja amepatikana na ameshatoa kiasi kidogo cha fedha.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania John Magufuli ameruhusu makontena yenye mchanga wa madini ya dhahabu kuuzwa, akibainisha kuwa tayari mteja amepatikana na ameshatoa kiasi kidogo cha fedha.

Mwaka 2017 Serikali ya Tanzania iliyashikilia na kuzuia makontena hayo ya mchanga kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyushwa ili kupata mabaki ya madini yaliyoshindikana baada ya hatua ya kwanza ya uchenjuaji kufanyika mgodini.

Akizungumza leo Ijumaa Januari 24, 2020 katika hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kamati ya madini ya Barrick yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema uuzwaji huo utakuwa na faida kwa sababu ya makubaliano hayo.

“Kwa kuanzishwa kwa Twiga (imeundwa baada ya makubaliano ya Serikali na kampuni ya Barrick)  sasa nataka kuwahakikisha kuwa yale makontena tuliyoyashika sasa mkayauze vizuri. Leo tumeanza ukurasa mpya,” amesema Rais Magufuli.

Huku akiihakikishia ulinzi kampuni ya Barrick Gold, Rais Magufuli amesema hakuweza kuvumilia kuwa rais huku rasilimali za Watanzania zikisombwa.

“Dhahabu iliwekwa Tanzania na siyo sehemu nyingine, aliyeiweka ana makusudi yake. Kwa hiyo ikisombwa bila Watanzania kupata faida ya hicho kinachosombwa, hicho ndio kinaumiza na ndiyo nilichosema kwamba siwezi kuwa Rais wa mali inayosombwa.”

“Wanawaambia ni mchanga mnakubali Polisi wanasindikiza. Sasa kama ni mchanga kwa nini usiende hivi na unalindwa na katika maeneo yale (kwenye migodi) watu wana njaa masikini, hawa dawa, hawana elimu. Hiyo haiko sawa,” amesema Magufuli.

Akifafanua zaidi kuhusu makontena ya mchanga huo, Rais Magufuli amesema yalishaanza kuuzwa na mteja alishapatikana.

“Ndiyo maana nimesema hata yale makontena mfanye utaratibu mzuri yarudi kwenye kampuni ya Twiga. Najua yalishauzwa na mteja yupo. Pamoja na stori kwamba yanapelekwa kwenye kuyeyushwa, siyo kweli. Yalikuwa yanauzwa yakiwa bado huko na mnunuzi ninamjua na alikuwa ameshalipa asilimia fulani.”

“Sasa kama huyo mnunuzi anakuja kununua anunue kwa sasa faida tunajua itapatikana. Wale ambao hawakuamini sasa waamini, tuendelee kushirikiana kwa faida ya sehemu mbili,” amesema.

Mgogoro kuhusu mchanga huo ulianza Machi 3, 2017, baada ya katibu mkuu wa Wizara Nishati na Madini kutoa taarifa ya zuio la usafirishaji nje mchanga wa madini yenye asili ya metali na hivyo Serikali ilipiga marufuku usafirishaji nje makinikia na madini.

Hata hivyo, Julai 20, 2017, makontena 104 ya makinikia ya kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Bulyanhulu Gol Mine (BGM)  yalikamatwa bandarini na kamishna mkuu wa TRA katika taarifa yake kwa BGM alitoa sababu mbalimbali za kukamatwa kwa makontena hayo.

Sababu hizo ni pamoja na kutoa taarifa ya uongo ya usafirishaji kwa kutojumuisha madini ya Rhodium, Iridium Sulphur, Tantalum, Iron, Lithium, Berullium na Tttebium na kutangaza uzito na thamani ya chini ya madini.

Nyingine ni usafirishaji haramu wa makusudi wa madini kinyume cha masharti na kwamba BGM ilifanya hivyo kinyume cha Sheria ya Usimamizi wa Masuala ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kutokana na hoja hizo, kamishna mkuu wa TRA chini ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi aliitaka kampuni hiyo kuwasilisha ushahidi wa taarifa mbalimbali.

Ushahidi huo ni hati halisi ya au iliyothibitishwa ya malipo mrabaha iliyoandaliwa na kusainiwa na mrufani, kutathmini na kulipa ada ya mrabaha wa madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyomo katika makontena 277 ya makinikia yaliyokuwa katika maghala yakisubiri kusafirishwa.

Vilevile risiti halisi au iliyothibitishwa ya malipo taslimu iliyotolewa kwa mrufani kuhusu malipo ya mrabaha wa madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyokuwemo kwenye makontena hayo.

Pia, kibali cha kusafirisha nje madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyokuwemo na fomu halisi au iliyothibitishwa ya maombi ya kusafirisha nje ya nchi madini mengine zaidi ya dhahabu, shaba na fedha yaliyokuwemo.

Vilevile aliomba nyaraka za tamko la kusafirisha nje ya nchi na kuhusu uzito wa makontena 277 ya makinikia kabla na baada ya kufungwa, na taarifa nyingine ambazo mrufani angeona kuwa ni muhimu kuthibitisha usafirishaji.

Aprili, 2019 Bodi ya Rufaa za Kodi (Trab) ilibariki uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuyashikilia na kuzuia kusafirishwa nje ya nchi makontena ya mchanga unaodaiwa kuwa na madini.

Novemba 29, 2017, BGM ilikata rufaa Trab dhidi ya kamishna mkuu wa TRA kupinga kukamatwa makontena yake 104 ya makinikia yanayodaiwa kuwa na dhahabu.

Ilikuwa ikidai kuwa makontena hayo yaliyokuwa bandarini kwa maandalizi ya kusafiishwa nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji yalikuwa yameshikiliwa kinyume cha sheria, kwani usafirishaji wa makinikia hayo ni kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Trab katika hukumu iliyotolewa na aliyekuwa mwenyekiti wake, Cyprian Mkeha baada ya kusikiliza rufaa hiyo ilikubaliana na hoja za TRA kupitia kwa wakili wake, Juma Beleko kuwa ilikuwa sahihi.

Katika uamuzi huo wa Trab uliosambazwa kwa wadau Alhamisi iliyopita imekubaliana na wakili Beleko kuwa makinikia yaliyokamatwa ni miongoni mwa bidhaa zilizozuiwa kwa mujibu wa kanuni za uchimbaji madini (Biashara ya Madini) chini ya kifungu cha 211 cha Sheria ya Uchimbaji Madini.