Magufuli ashauri kuachiwa mahabusu wa uhujumu uchumi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) nchini humo kwenda magerezani ndani ya siku saba kuanzia kesho Jumatatu kuwasikiliza mahabusu wa makosa ya utakatishaji fedha walio tayari kurejesha fedha na kuomba msamaha ili waweze kuachiwa.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameshauri mahabusu wa makosa mbalimbali hasa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurudisha fedha walizotakatisha, wasikilizwe ndani ya siku saba kesho Jumatatu Septemba 23 hadi Jumamosi ya Septemba 28, 2019.

Magufuli ameyasema hayo leo Jumapili Septemba 22, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua Ijumaa iliyopita ya Septemba 20, 2019.

Kiongozi huyo wa Tanzania amerejea kauli aliyowahi kuitoa huko nyuma kwamba hapendi kuongoza taifa la watu wenye machungu hususan waliopo magerezani huku akitamani siku moja kusiwe na mahabusu wala wafungwa.

“Mimi naumia kuona watu wapo mahabusu au watu wamefungwa. Ni bahati mbaya kwa sababu sheria zipo. Lakini mtu anapowekwa mahabusu inaumiza sana,” amesema Magufuli.

Kutokana na hilo, Magufuli amemwagiza Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Biswalo Mganga na wote wanaohusika na sheria kuwasikiliza mahabusu wenye kesi za uhujumu uchumi ambazo hazitawafanya kutoka mapema kwa mujibu wa sheria na kama itaruhusu watoke.

Amewataka kutengeneza mazingira watu hao warudishe fedha zote walizochukua kwa sababu wanateseka kukaa mahabusu miaka hadi mitatu na wengine wamekonda.

“Najua wanateseka, unawaona wanavyopelekwa mahakamani, wengine wamekonda kweli inatia huruma inaumiza. Najua wengine wanataka kuomba msamaha waje kwako DPP mpange warudishe,” amesema Magufuli

 

 

 

Magufuli ametoa mapendekezo kwa wanasheria kuwa waliotakatisha fedha watubu kosa hilo na kutaka kufanya biashara halali ili watoke.

”Mtu anaweza kutubu akarudisha hiyo hela tukaitumie katika maendeleo mengine, ikajenge hospitali, ikanunue madawa, ikawasaidie watoto,” amesema Rais Magufuli.

Amesema kwa wale ambao hawataomba msamaha ndani ya siku saba waendelee kuwabana hata kama kesi itachukua miaka 20.

Magufuli amesema Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, Kamishna Jenerali Phaustine Kasike alimuomba askari 800 na hakumjibu.

Amesema angekuwa na uwezo ingetokea siku moja kusingekuwa na mfungwa wala mahabusu ili askari magereza wafanye kazi nyingine.

“kwa hiyo yeye anataka niongeze wafungwa kule. Kwa kweli sikupi. Mimi nataka wapungue tuje kuijenga Tanzania yetu,” amesema