Magufuli ataja sababu kutumia magari ziara yake mkoani Lindi

Muktasari:

Rais wa Tanzania,  John Magufuli amesema anatumia usafiri wa magari katika ziara zake mkoani Lindi ili kujionea changamoto katika barabara anazopita na kujua hali halisi za wananchi, kutatua kero zinazowakabili.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,  John Magufuli amesema anatumia usafiri wa magari katika ziara zake mkoani Lindi ili kujionea changamoto katika barabara anazopita na kujua hali halisi za wananchi, kutatua kero zinazowakabili.

Amesema katika kutimiza hilo atashirikiana na

mawaziri, viongozi wengine wa Serikali kuhakikisha anatimiza aliyoahidi kwa wananchi katika kipindi cha utawala wake.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 16, 2019  aliposimama kijiji cha Ikungu wilayani Nachingwea kusalimia wananchi akiwa katika ziara yake mkoani Lindi.

“Nitaendelea kuchapa kazi kwa kushirikiana na mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi makatibu tarafa na ma DAS (makatibu tawala wa wilaya) nataka niwahakikishie muendelee kuwa wamoja, mchape kazi tuendelee kumshirikisha Mungu.”

“Nimepita barabara hii niione mimi mwenyewe kwa macho yangu mpaka nitakapofika nijue changamoto zinazowakabili,  ninyi wananchi niweze kufanya maamuzi sahihi, kila ninapopita naona kuna shule za msingi na sekondari na elimu ni bure hivyo naomba vijana msome kwa bidii,” amesema Rais Magufuli.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema, “Wilaya hii tumewekeza Sh400 milioni kwenye ujenzi wa kituo cha afya Malondo,  kwa sasa kipo katika hatua ya kukamilika.”

“Hospitali ya wilaya wodi kubwa ya kisasa huduma ya mama na mtoto tunataka kundi hili wapate huduma safi na tunaahidi tutawaletea vifaa, kuna changamoto ya huduma ya X-Ray, chumba cha meno na gari la wagonjwa mheshimiwa Rais ameahidi fedha itatolewa na huduma hizo zitaletwa.”