VIDEO: Magufuli ataja sifa za Mwalimu Nyerere

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema mwalimu Julius Nyerere alikuwa kiongozi mahiri, shupavu na jasiri aliyeiongoza nchi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema mwalimu Julius Nyerere alikuwa kiongozi mahiri, shupavu na jasiri aliyeiongoza nchi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Oktoba 14, 2019 katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha Nyerere yanayofanyika katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano itajitahidi kumuenzi Nyerere bila woga wowote na imekuwa ikifanya hivyo kwa kutekeleza mambo aliyoasisi ikiwamo kufanya kazi kwa uadilifu.

Magufuli amesema Nyerere aliamini njia pekee ya kuleta ukombozi wa kiuchumi na kulinda uhuru wa kisasa nchini ni kujenga Taifa la kijamaa linalojitegemea, kwamba kupitia Azimio la Arusha alihimiza watu kufanya kazi kwa bidii.

“Alisema wazee wasiojiweza na watoto pekee ndio wanaopaswa kuishi kwa jasho la wengine, ndio dhana ya uhuru na kazi ikainuka,” amesema Rais Magufuli.

Amesema Nyerere alisisitiza elimu kwa wote hasa kwenye ufundi kama njia ya kukuza ujuzi na teknolojia ya uzalishaji.

“Aliamini ili watanzania watumie vizuri maliasili na raslimali zao ni lazima wawe na elimu ya kutosha ndio maana alitaka raslimali na madini zisitumike mpaka pale watakapokuwa tayari,” anaeleza Rais Magufuli.

Amebainisha kuwa mwalimu Nyerere hakuwa na mchezo na watumishi waliojihusisha na ufisadi wa mali za umma na yeyote aliyefanya hivyo aliingia na kutoka jela kwa fimbo.

“Kutokana na mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere watanzania wanakila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kumfanya kiongozi huyo azaliwe Tanzania,” amesisitiza.

Amempongeza Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kwa kutenga siku maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya mwalimu Nyerere na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuendeleza siku hiyo.