Breaking News

Magufuli afungua pazia la kampeni, ataja vipaumbele 25

Monday August 24 2015

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akihutubia wafuasi wa chama hicho waliofurika katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amefungua pazia la kampeni za chama hicho kwenye Viwanja vya Jangwani katika tukio lililohudhuriwa na maelfu ya wananchi, huku akieleza mambo 25 atakayoyafanya iwapo Watanzania watamchagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano.

Huku akitumia maneno: “Mimi kazi tu”, “Tanzania ya Magufuli ni ya viwanda”, Dk Magufuli aliyetumia dakika 53 kueleza sera zake, kuanzia saa 11.40 hadi 12.33 jioni alisema Watanzania wanataka kitabu kipya cha mabadiliko na yeye na mgombea mwenza, Samia Suluhu ndiyo wanaoweza kuyaletea.

Mgombea huyo wa urais wa CCM aliahidi kuanzisha mahakama maalumu ya kusikiliza kesi za rushwa na ufisadi, kumaliza tatizo la wanafunzi wa elimu ya juu kukosa mikopo, kuhakikisha mama lishe hawabughudhiwi, kusimamia haki za wasanii, kulinda Muungano na usalama wa nchi.

Aliahidi kutoingilia utendaji kazi wa Bunge na Mahakama, kuheshimu mawazo ya vyama vingine vya siasa, kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara wadogo na wakubwa wote kulipa kodi, kuendeleza kilimo, mifugo, uchimbaji wa madini, majisafi na elimu bora.

Nyingine ni kusimamia nishati ya gesi, ujenzi wa barabara, reli, kuboresha sekta ya utalii, kuimarisha uwekezaji, kuwasaidia walemavu na kusimamia uhuru wa habari.

Mkutano huo ulioanza rasmi saa 9.30 alasiri ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Salim Ahmed Salim.
Ahadi alizotoa

Advertisement

Mgombea huyo alitoa ahadi mbalimbali ikiwamo ajira akisema: “Ninataka Watanzania wapate ajira, kazi ya Serikali itakuwa kukusanya kodi tu. Viwanda vinaweza kutengeneza ajira kwa asilimia 40 hasa kwa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini.”

Kuhusu ubinafsishaji, alisisitiza: “Kuna viwanda vilibinafsishwa sasa wahusika wasipoviendeleza wajiandae kuvirudisha haraka.”

Mbali na kurejesha viwanda vilivyobinafsishwa, alisema akipewa ridhaa hiyo atahakikisha chini ya uongozi wake, anajenga viwanda vingi vipya, akiainisha vile mahsusi kwa shughuli za kilimo, mifugo, kusindika nyama na madini.

Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kilimo na kwamba atahakikisha sekta hiyo ambayo ndiyo mhimili wa uchumi inaendelezwa.

“Tutaleta vitendea kazi, pembejeo na vifaa vingi vya kisasa na vya kutosha kwa wakulima… kama nilivyosema hapo awali, tutajenga viwanda kwa ajili ya wakulima pia.

Mbunge huyo wa zamani wa Chato alisema pia kipaumbele kingine katika Serikali yake ni kuhakikisha kuwa wananchi wa mjini wanapata majisafi na salama kwa asilimia 95 na wananchi wa vijijini wanapata maji kwa asilimia 85.

Kuhusu afya alisema: “Tutahakikisha tunakuwa na vituo vya afya, zahanati na hospitali katika maeneo mbalimbali kwa sababu tunaamini maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana kama wananchi hawana afya bora.”

Kipaumbele kingine ni mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu akisema watakuwa wanapata mikopo kwa wakati bila kuchelewa na kwamba watajikita pia katika kujenga hosteli kwa wanafunzi wa vyuo.

“Mishahara ya walimu na wafanyakazi wote tutaishughulikia. Hata madereva haki zao za msingi lazima ziangaliwe,” alisema huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Mgombea huyo alisema anafahamu kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na kwamba maendeleo ya kweli yatapatikana kama changamoto hiyo itafanyiwa kazi.

“Tutaunganisha mikoa yote kwa barabara zenye viwango vya lami na pia tutajenga barabara za juu saba jijini hapa,” alisema Magufuli.

Alisema akipewa ridhaa hiyo itashughulikia suala la reli  kwa kujenga reli ya kisasa kwa viwango vya Standard Gauge” na kuboresha bandari na usafiri wa anga.

Kuhusu maliasili, alisema ni kipaumbele katika Serikali yake endapo akipewa ridhaa ya kuongoza nchi huku akieleza kukerwa na ujangili... “Ninapata shida sana ninapoona meno ya tembo yanauzwa Ulaya halafu unaambiwa yanatoka Tanzania… sasa unajiuliza yanapitaje?”

Alisema ili kushughulikia suala hilo atahakikisha watendaji wa sekta hiyo wanaboreshewa masilahi yao ili wachangie mapato ya nchi.

Aliahidi Serikali yake kuwa rafiki wa wawekezaji na kwamba italinda masilahi ya wafanyabiashara.

Mgombea urais huyo aliahidi kuwa atalinda uhuru wa habari na atafanya kazi na waandishi wa habari siyo tu wakati wa kipindi cha kampeni, bali hata baada.

Katika ahadi zake, Dk Magufuli hakuwaacha wasanii, alisema atahakikisha wanapata hakimiliki na kuhakikisha wao pamoja na wanamichezo wanaanzishiwa mfuko kwa ajili ya kuwasaidia katika mambo mbalimbali.

Soma zaidi habari hii kupitia Mwananchi E-paper

Advertisement