Rais Magufuli ataka viongozi wa dini kuwaombea maofisa upelelezi

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaomba viongozi wa dini kuwaweka kwenye maombi maofisa upelelezi ambao ni chanzo cha mlundikano wa mahabusu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewaomba viongozi wa dini kuwaweka kwenye maombi maofisa upelelezi ambao ni chanzo cha mlundikano wa mahabusu.

Amesema mlundikano huo unasababisha mahabusu kunyimwa haki zao.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 6, 2020 katika maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema wapelelezi wanakwamisha kesi za watu jambo linalorudisha nyuma jitihada za kupunguza msongamano wa mahabusu katika magereza.

Amesema kwa sasa kuna mahabusu 17,632 kiasi ambacho ni kikubwa na kimetokana na uzembe unaofanywa na wapelelezi.

“Wapelelezi wanachelewesha kesi kwa makusudi utasikia upelelezi haujakamilika. Wakati mwingine hata kupelekwa mahakamani ni lazima uhonge ili kesi yako isomwe. Badilikeni, viongozi wa dini kaliombeeni sana suala hili ili wanaochelewesha kwa makusudi wakapate laana.”

“Ninaomba wapelelezi na wasimamizi wa sheria mlifanyie kazi, ukienda kwenye Magereza watu wanalia. Kuna watu wamewekwa mule kwa sababu ya matajiri wakiwaambiwa watawakomesha,” amesema Magufuli.