Magufuli ataka wanaoihusisha Tiss na watu kupotea wakamatwe

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwashtaki watu wanaovihusisha vyombo vya ulinzi na usalama ikiwamo Idara ya Usalama wa Taifa (Tiss) na matukio ya kupotea na kutekwa kwa watu.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Ijumaa iliyopita alipokuwa akiweka jiwe la msingi jengo la Idara ya Usalama wa Taifa eneo la Maisara, Zanzibar ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi Zanzibar zilizofanyika jana.

“Tunasema tuko salama, lakini ni kwa sababu kuna watu fulani wanateseka, wapo watu hawalali, wapo watu wanafikiria, wapo watu saa nyingine wanatukanwa hawajibu, kwa sababu siku hizi kumekuwa na tabia ya hovyo ambayo imejitokeza kwa baadhi ya Watanzania wachache.” alisema.

“Kila kitu kinachofanywa ni Usalama wa Taifa, mtu akipotea hata siku mbili hata kama hajapotea yuko kwa mpenzi wake ni Usalama wa Taifa. Saa nyingine mtu anatoroka kidogo anakwenda kwa mganga wa kienyeji, ni Usalama wa Taifa,” alisema Rais Magufuli.

Amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutofumbia macho tuhuma hizo kwani zinapotosha ukweli na kuchafua taswira ya vyombo hivyo.

“Mahali popote vyombo vya ulinzi na usalama, Taifa lolote ni ‘number one’ katika kupewa heshima. Sasa niviombe vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, ikiwamo Polisi ambao mnashughulikia wahalifu, msiwaache wahalifu waanze kuchafua ulinzi na usalama, mwelekeo wake ni mbaya.”

“Mtu akizungumza amepotea huyu, mshikeni mpaka atoe ushahidi, asipotoa ushahidi, lazima sheria zichukue mkondo wake.”

“Ninajua IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi- Simon Sirro) unanisikia, haiwezekani vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotufanya sisi tuwe salama pamoja na wao, vinakuwa kila siku ni kejeli na kutukanwa. Nitalisimamia na katika kusimamia ni pamoja na kuwalinda Watanzania wote pamoja na kulinda vyombo vya ulinzi na usalama visidharaulike,” alisema.

Waliopotea

Kauli ya Rais Magufuli imekuja wakati kukiwa na matukio kadhaa ya watu kudaiwa kutekwa na kupotea na wengine wakijeruhiwa na kuuawa na watu ‘wasiojulikana’.

Miongoni mwa watu waliopotea ni pamoja na Simoni Kanguye, Ben Saanane, Azory Gwanda, na wengine ambao walipotea kwa muda na kupatikana ni mwanafunzi Idrissa Ally na mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji, ‘Mo Dewji’.

Ben Saanane aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18, 2016 na haijafahamika kama alitekwa au kupotea.

Mwingine ni Kanguye, ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo mkoani Kigoma aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 20, 2017.

Azory Gwanda, ambaye ni mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) mkoani Pwani alichukuliwa na watu wasiojulikana Novemba 21, 2017.

Kwa mujibu wa mkewe Anna Pinoni (35), siku hiyo asubuhi watu wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, walifika katikati ya mji wa Kibiti sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara na kumchukua.

Mbali na watu waliopotea, Mo Dewji aliyetekwa jijini Dar es Salaam alipatikana baada ya siku 10. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa katika taarifa za awali alidai waliomteka Mo Dewji walikuwa ni raia wa kigeni.

Kutekwa kwake kuliifanya familia ya Mo Dewji ambaye ni miongoni mwa mabilionea vijana Afrika itangaze donge la Sh1 bilioni kwa yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake.

Hata hivyo, Mei 28 mwaka jana, Jeshi la Polisi lilimfikisha mahakamani dereva teksi, Mousa Twaleb akihusishwa na tukio la kutekwa kwa Mo.

Maoni ya wadau

Akizungumzia kauli ya Rais, mwanasheria maarufu nchini, Fatma Karume alisema vyombo vya ulinzi na usalama vina wajibu wa kuwakamata watekaji.

“Ukweli ni kwamba kuna watu wengi nchi yetu wamepotea... Kila watu wakilalamika polisi wanasema hayo mambo yamefanywa na watu wasiojulikana. Watu wanaotoa ushahidi wakisema kuna watu wamekuja kuchukuliwa nyumbani na wamejitambulisha kuwa ni Usalama wa Taifa,” alisema.

Huku akitoa mfano wa kupotea kwa mwandishi Azory Gwanda alisema haitakuwa haki kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata watu wanaotoa taarifa.

“Huwezi ukamkamata mtu aliyetoa ripoti. Hata kama siyo Usalama wa Taifa, watafutwe wanaoteka watu, maana siyo wananchi wanaoharibu sifa ya vyombo vya usalama bali ni hao wanaopita nyumbani kwa watu kuteka watu. Kwa nini uwakamate watoa taarifa? Kuna kosa gani kutoa taarifa?” Alihoji na kuongeza: “Sheria zetu zinasema, kila mwananchi anayeona uovu ana wajibu wa kutoa taarifa. Kutoa taarifa ni wajibu wa kisheria na siyo jinai.”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa aliungana na kauli ya Rais Magufuli akisema, “sina tatizo na kauli ya Rais kwani hata sisi tunasema mtu asikamatwe bila upelelezi kukamilika, vivyo hivyo usishutumu mtu au vyombo vya dola kama huna ushahidi.”

Ole Ngurumwa alisema ili kuondoa minong’ono ya hapa na pale, “Watu ambao wamekuwa wakipotea na kurudi basi wawe wanaeleza ukweli na wasikae kimya ili Watanzania waweze kujua.”

Alisema kauli ya Rais Magufuli haijazuia mtu akipotelewa asitoe taarifa au kusema kuwa amepotelewa, “lakini anachojaribu kusema Rais Magufuli, tusituhumu kama hatuna ushahidi.”