Magufuli ateua viongozi wa tume ya haki za binadamu

Sunday September 22 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemteua Jaji mstaafu Methew Mwaimu kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Jaji Mwaimu anachukua nafasi iliyokuwa wazi tangu mwanzoni mwa mwaka 2018 baada ya Bahame Nyanduga aliyekuwa mwenyekiti kumaliza kipindi chake cha uongozi.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Septemba 22,2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imemnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akisema pamoja na uteuzi wa Mwenyekiti, Rais Magufuli amemteua Mohamed Khamis Hamad ambaye ni Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar kuwa Makamu Mwenyekiti wa  tume hiyo.

Pamoja na uteuzi huo, Rais Magufuli ameteua Makamishna wa Tume hiyo kama ifuatavyo; Dk Fatma Rashid Khalfan (Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar), Thomas Masanja (Mhadhiri wa Sheria, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino – SAUT) na Amina Talib Ali (Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar).

Pia, amemteua Khatib Mwinyi Chande (Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Huria Tanzania – OUT) na Nyanda Josiah Shughuli (Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango).

Balozi Kijazi amesema uteuzi huo umeanza  Septemba 19 2019.

Advertisement

Advertisement