VIDEO: Magufuli atoa mwezi mmoja wasiotumia TTCL serikalini kuanza mara moja

Muktasari:

Rais John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa ofisi yake na wizara mbalimbali ambazo bado hazijaanza kutumia huduma za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuanza kutumia.

 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa ofisi yake na wizara mbalimbali ambazo bado hazijaanza kutumia huduma za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuanza kutumia.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 21, 2019  ikiwa ni muda mfupi baada ya kusomwa kwa majina ya ofisi zinazotumia mtandao wa mawasiliano wa TTCL, huku ofisi ya Rais ikiwa miongoni mwa zinazotumia mtandao huo.

Akizungumza katika hafla ya kupokea gawio la TTCL walilolitoa serikalini, Rais Magufuli amesema mbali na ofisi yake pia amesikitika kutosikia Chama cha Mapinduzi (CCM) kutumia mtandao huo licha ya kuwa katibu mkuu wake, Dk Bashiru Ally ni mzalendo.

“Inaonekana hawa wanapinga hata kwenye ofisi yangu wamo, sasa kama wananisikia au kama huwa wananisindikiza sindikiza nataka katika kipindi cha mwezi mmoja tuanze kutumia simu za TTCL.”

“Siyo ofisi ya rais, siyo wizara ya fedha, maana yake tunazungumza maneno zaidi kuliko vitendo, sasa sifahamu wafanyakazi wenzangu wa TTCL sijui nifanye nini hapa. Mimi nina laini ya TTCL najilipia mwenyewe lakini naweza kumuuliza mwenyekiti wa kamati ya miundombinu ukakuta hana laini ya TTCL,” amesema Magufuli.

Ameongeza, “Ni lazima tuwe wazalendo kwa sababu bila kufanya hivyo tutachezewa mno, tusipowaimarisha hawa TTCL hatutafika sehemu yoyote. Sijasema msiwe na laini nyingine lakini kwa kuna ubaya gani serikalini wakasema ukitaka kulipiwa simu ni TTCL.”

“Wakati mwingine kujipa amri ni shida ila ngoja nijipe tu, ndani ya mwezi mmoja na wizara nyingine ambazo hamjafanya hivyo muwe mmeanza kutumia TTCL.”