Magufuli atoe neno uchaguzi serikali za mitaa

Muktasari:

Oktoba mwaka 2019, Tanzania itafanya uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo Rais wa nchi hiyo, John Magufuli ametoa wito kwa wananchi kuchagua viongozi watakaozingatia maadili na kumshauri vyema ili kuwaletea maendeleo

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka Watanzania kutumia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba mwaka 2019 kuwachagua viongozi wazuri na sio watoa rushwa.

Magufuli ametoa wito huo leo Jumatatu Julai 15,2019 wakati akizungumza na wananchi wa Katoro na Buselesele mkoani Geita akiwa njiani kuelekea Magogo Geita ambako atazindua nyumba za askari wa jeshi la polisi.

“Mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mitaa, chagueni viongozi wazuri, msichague viongozi wanaowapa rushwa, mkikosea kuchagua madhara yake ni makubwa.”

“Mkasimame imara katika kuchagua viongozi ambao mnafikiri wataweza kunisaidia pia na kunishauri vizuri,” amesema

Rais Magufuli pia amesisitiza wakazi wa maeneo hayo kudumisha amani, upendo na umoja na kutokubali kufarakanishwa.

“Msikubali watu kuwatofautisha, endelezeni misingi ya amani na umoja aliotuachia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere,” amesema

Pia, Rais Magufuli amewaeleza wakazi hao kuwa ombi lao la kupandishwa hadhi amelipokea, “Hii Buselesele inatakiwa kuwa zaidi ya kata, inatakiwa kuwa juu zaidi, nafikiri mmenielewa.”