Magufuli atoa sababu ya kumtengua aliyetangaza Tanzania kuna Zika

Muktasari:

Rais John Magufuli wa Tanzania leo Ijumaa ameanza ziara ya siku tisa katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi. Akiwa Songwe amezungumzia suala la ugonjwa wa zika uliomfanya kumchukua hatua bosi wa NIMR.

Mbozi. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema katika kipindi ambacho nchi inapiga hatua kuelekea uchumi wa kati nchi itazushiwa magonjwa ya kila aina na ya kutisha kwa vile mabepari walizoea kuinyonya na hawapendi kuona inajitegemea.

Magufuli amesema hayo jana Ijumaa Oktoba 4, 2019 alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mji wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Songwe.

Rais Magufuli alitumia mkutano huo kuzungumzia sababu zilizomfanya kumfukuza kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyotoka Desemba 16, 2016 ilielezea Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Dk Mwele pasina kueleza sababu.

Leo Ijumaa katika mkutano wake, Rais Magufuli hakumtaja kwa jina Dk Mwele ambapo alisema unapojenga miradi mikubwa kwa fedha za ndani, kununua ndege kwa fedha tasilimu, kujenga reli ya kisasa na kugharamia elimu bure mabeberu hawawezi kupenda.

Amesema ni lazima watafute kila njia ya kuwakwamisha kwa kuwazulia magonjwa makubwa na ya kutisha ili kusudi msiende mbele kama ambavyo mmekuwa mkisikia.

“Kuna wakati fulani tuliambiwa hapa Tanzania tuna Zika, alipozungumza hivyo na kwa sababu nilikuwa najua hakuna zika, niliposikia hivyo aliyetangaza nikamfukuza, nilimfukuza nakumbuka saa 7.30 usiku.”

“Wala hakuna cha zika iliyotokea, yule niliyemfukuza baada ya wiki akateuliwa, ina maana walimtuma kutangaza,” amesema Rais Magufuli

Amesema, “ukishakuwa na zika watu hawatakuja katika nchi yako, hawatakuja kuwekeza, hizo ni mbinu za kibeberu.”

Aprili mwaka 2017, Aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika vya Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, salamu za pongezi zimeendelea kumiminika.

Dk Mwele aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mpango wa Maalumu wa WHO wa kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele kanda ya Afrika (Espen) ambapo kituo chake cha kazi Congo-Brazaville.

Mradi wa Espen ulianza kutekelezwa mwaka 2016 hadi 2020, una lengo la kumaliza magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwa kutoa vifaa tiba, elimu na dawa.

Magonjwa yasiyopewa kipaumbele ni pamoja na matende, mabusha, kichocho, minyoo ya tumbo na usubi.