VIDEO: Magufuli atuma salamu za rambirambi ajali iliyoua 18 Mkuranga

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa watu takribani 18 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea leo asubuhi Jumatatu Aprili 15, 2020 katika kijiji cha Kilimahewa Kaskazini Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa watu takribani 18 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea leo asubuhi Jumatatu Aprili 15, 2020 katika kijiji cha Kilimahewa Kaskazini Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Ajali hiyo imehusisha basi dogo la abiria lililokuwa likitoka kijiji cha Magawa wilayani Mkuranga kwenda jijini Dar es Salaam ambalo limegongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kusini.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu imemnukuu Magufuli akimtaka mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kufikisha salamu zake za pole kwa familia za marehemu na ameeleza kwamba anaungana nao katika kipindi hiki cha majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao.

Nawaombea familia za marehemu wote, ndugu, jamaa na marafiki kuwa na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, kuwapoteza Watanzania wenzetu kwa idadi kubwa namna hii inaumiza sana, ” amesema Magufuli.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amevitaka vyombo vya usalama barabarani kuhakikisha vinachukua hatua madhubuti za kuzuia ajali za barabarani na amewataka madereva na wote wanaotumia barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali ambazo zinagharimu maisha ya watu na uharibifu wa mali.