Magufuli awakemea wanaofanya hujuma dhidi ya Serikali

Rais wa Tanzania, John Magufuli

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kuna watu wanafanya hujuma  kwa ajili ya kujinufaisha wao  na kufifisha jitihada za Tanzania kujikomboa kiuchumi.

 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kuna watu wanafanya hujuma  kwa ajili ya kujinufaisha wao  na kufifisha jitihada za Tanzania kujikomboa kiuchumi.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 12, 2019  wakati akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM jijini Mwanza.

“Hujuma dhidi ya jitihada za Serikali zinazofanywa na baadhi watu wasioitakia mema serikali, hujuma hizi zinalenga kufifisha jitihada zetu za kujikomboa kiuchumi kwa maslahi yao binafsi.”

“Watu hao kamwe hawataki kuona tunadhibiti rasilimali zetu ambazo walikuwa wanazivuna na kuzisafirisha wanavyotaka bila kuulizwa na mtu,” amesema Magufuli.

Ameongeza, “Hawatakubali tutekeleze miradi mikubwa ya kimapinduzi inayoharakisha maendeleo nchini ikiwemo bwawa la Nyerere. Wasingependa miradi mikubwa, tutoe elimu bure kwa watoto wetu hata tupeleke vijijini umeme wa kutosha.”

Amesema watu hao wanataka wategemewe wao wakati wao wanaishi kwa kutegemea rasilimali za Tanzania.

“Wakati mwingine watatumia asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali kujifanya wanatufundisha demokrasia na haki za binadamu wakati wao wanavunja misingi hiyo kwa kujenga mifumo ya kinyonyaji kwa kuchochea machafuo na kuingilia uhuru wa mataifa mengine,” amesema Magufuli.

Ameongeza, “watajenga mazingira ya taharuki wanaweza kukwambia una ebola ilimradi tu ionekane nchi haiko salama, inatupasa kutambua kuwa hii ndio changamoto kubwa katika mapito yetu kuelekea ukombozi wa uchumi.”