VIDEO: Magufuli awaonya vigogo polisi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka maofisa wa polisi kuwaacha askari wa vyeo vya chini kufanya shughuli zao

Dodoma. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka maofisa wa polisi kuwaacha askari wa vyeo vya chini kufanya shughuli zao.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 22, 2019 wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa nyumba za askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)  zilizopo Nzuguni mjini Dodoma.

Magufuli amesema maofisa hao wanatoa maagizo askari wa vyeo vya chini wanapowakamata watuhumiwa .

“Tuwaache askari wa chini wafanye kazi nadhani ujumbe umefika,” amesema Rais Magufuli.

Amesema atafanya mkutano na askari wa vyeo vya chini  bila kuwepo kwa maofisa wao ili wazungumze mambo yanayowahusu.

Leo kiongozi huyo ametoa jengo la ghorofa nne la Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) lilipo mjini Dodoma kwa Jeshi la Polisi ili litumike kama makao makuu yao.

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amesema uhalifu umepungua katika miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli.

Amesema kushuka huko kwa uhalifu kunatokana na mafunzo kwa watendaji, vifaa na motisha kwa Jeshi hilo.

Amesema makosa ya jinai yamepungua kwa asilimia 24.9, unyang’anyi wa kutumia nguvu asilimia 54.2 na makosa ya barabarani kwa asilimia 69.4.