VIDEO: Magufuli awapa wiki moja mabalozi wapya kuondoka Tanzania

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapa wiki moja mabalozi watano aliowaapisha leo Jumamosi Novemba 23, 2019 kukamilisha taratibu za kuaga na kuondoka nchini kwenda kwenye vituo walivyopangiwa.


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapa wiki moja mabalozi watano aliowaapisha leo Jumamosi Novemba 23, 2019 kukamilisha taratibu za kuaga na kuondoka nchini kwenda kwenye vituo walivyopangiwa.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa agizo hilo muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya kuwaapisha mabalozi hao Ikulu Chamwino, mjini Dodoma.

“Samahani kidogo kwa mabalozi walioteuliwa, kumekuwa na tabia mkishateuliwa mnakaa miezi mnakwenda kuaga kwenye maofisi, leo ni juma ngapi?”

“Leo ni Jumamosi, ninawapa wiki moja tu muwe mmeshaondoka Tanzania kwenda kwenye sehemu zenu.”

Ameongeza, “nataka niwaeleze wazi kwa sababu mmeshateuliwa muende mkafanye kazi, imekuwa ni tabia leo niko kwenye ofisi ya waziri nani, nakwenda wapi, hapana. Tumeshamaliza maagizo hakuna kwenda kuaga kazini. Mungu awajalie,” amesema Magufuli.

Mabalozi walioapishwa katika hafla hiyo ni Meja Jenerali Anselm Shigongo Bahati (Misri), Mohamed Abdallah Mtonga (Abu Dhabi), Jestas Abouk Nyamanga (Ubelgiji),  Ali Jabir Mwadini (Saudi Arabia)  na Dk Jilly Elibariki  (Burundi).