Magufuli ataka askari wanane walioachiwa huru kurejeshwa kazini

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli ameagiza askari polisi wanane waliofutiwa kesi kuhusiana na shehena ya dhahabu na rushwa ya Sh305 milioni kurejeshwa kazini huku akiwaagiza polisi kutojihusisha na rushwa, kuonea na kuwabambikia kesi raia


Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameagiza askari wanane waliochiwa huru leo Alhamisi Julai 18, 2019 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza baada ya kufutiwa kesi iliyokuwa ikihusiana kusafirisha shehena ya dhahabu na rushwa ya Sh305 milioni warejeshwe kazini.

Akihutubia wananchi wa Kongwa jijini Dodoma katika mkutano unaorushwa moja kwa moja kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania TBC, Rais Magufuli amewaagiza askari hao ambao walishafukuzwa kwenda kuchapa kazi.

"Nawataka polisi wajiepushe na vitendo vya rushwa, kuonea na kubambikia kesi watu wasio na hatia," amesema Rais Magufuli

Hata hivyo, kiongozi huyo mkuu wa nchi hakutaja sababu za kuachiwa huru kwa askari hao ambao awali Januari mwaka 2019 alilieleza Taifa kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuhusu walivyohusika kwenye tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.

Askari hao walioachiwa huru ni Mkuu wa Operesheni mkoa wa Mwanza, Morice Okinda, E 6948 D/CPL Kasala, F 1331 PL Matete, G 6885 D/C Alex na G 5080 D/C Maingu, G 7244 D/C Timothy, G 1876 D/C Japhet, H 4060 D/C David Kadama

Askari hao walifikishwa mahakamAni hapo kwa mara ya kwanza Januari 11, 2019 ambapo kwa pamoja na wafanyabiashara wanne walikuwa wakikabiliwa na makosa matano ya kutakatisha fedha, uhujumu uchumi na kula njama za kupanga uhalifu, makosa waliyodaiwa kuyatenda kati ya Januari 4 na 5, 2019.

Kutokana na mashtaka hayo kutokuwa na dhamana, askari hao na wenzao walikuwa katika gereza la Butimba Mwanza.