VIDEO: Magufuli azindua kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi Kilimanjaro

VIDEO: Magufuli azindua kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi Kilimanjaro

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema atashangaa viongozi wa serikalini, viongozi wa kitaifa na wanafunzi kama wataendelea kuvaa viatu vinavyozalishwa nje ya nchi badala ya vinavyozalishwa na viwanda vya ndani

 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema atashangaa endapo viongozi wa serikalini, viongozi wa kitaifa na wanafunzi wataendelea kuvaa viatu vinavyozalishwa nje ya nchi badala ya vinavyozalishwa na viwanda vya ndani.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 22, 2020 alipokuwa akizindua kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo mkoani Kilimanjaro huku kikiwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya jozi milioni 2 za viatu kwa mwaka.

Amesema kuanzishwa kwa kiwanda hicho kunatakiwa kupunguza uingizaji wa viatu kutoka nje ya nchi na badala yake vitumike zaidi vinavyozalishwa nchini.

Mahitaji ya viatu nchini ni jozi milioni 54 na viwanda vitano vilivyokuwapo vilikuwa vikizalisha jozi zaidi ya milioni 1.715 jambo ambalo lilikuwa likiifanya nchi kutumia fedha nyingi kuagiza viatu nje ya nchi ili kukidhi mahitaji, amesema Rais Magufuli.

“Na sasa kiwanda hiki kitazalisha jozi karibu milioni 2 kwa mwaka kitapunguza mahitaji ya viatu kutoka nje na kuanza kwake kazi kutapanua soko la ngozi kwa wafugaji,”

 “Sasa hadi kufikia hapa nitashangaa sana Mawaziri wakiongozwa na mimi Rais, Makamu wa Rais, mawaziri, makatibu wakuu tusianze kuvaa viatu vya hapa vinavyotengenezwa Kalanga,” amesema Magufuli

“Lakini nitashangaa na viongozi wengine wa kitaifa wanaoipenda nchi yao wasianze kuvaa viatu vinavyotengeneza hapa,”

Alitumia nafasi hiyo kuwataka wafugaji kuhakikisha ngozi wanazozizalisha zinakuwa na ubora ziweze kukidhi soko la kimataifa katika utengenezaji wa bidhaa za viatu, pochi, mikanda na bidhaa nyingine

“Tanzania ni wa pili duniani kwa kuwa na mifugo mingi lakini soko la ngozi kwa nchi yetu lilikuwa chini, wafugaji walikuwa wakitupa ngozi kwa sababu hakukuwa na soko,”

“Sasa uwepo kiwanda hiki na vingine soko la ngozi litakuwa limepatikana kwa wafugaji wanaozunguka eneo hili,” amesema Magufuli.

Aliwataka wazalishaji wa viatu katika eneo hilo kuzalisha bidhaa zenye ubora ili watu waweze kununua.

“Niwahimize Watanzania kuanza kununua bidhaa za ngozi zinazotengenezwa na kiwanda hiki tukianzia na viongozi wa Wizara husika na watendaji wao ili watuonyeshe mfano na biashara ni matangazo.”

“Niwahimize Watanzania wenzangu tupende vya kwetu na nitashangaa sana kama vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vitaendelea kuagiza viatu kutoka nje nitashngaa sana wanafunzi waendelee kuvaa viatu vya nje,” amesema Rais Magufuli.