Magufuli azindua kiwanda cha nafaka

Muktasari:

Rais Magufuli amezindua kiwanda cha kuchakata mahindi mkoani Ruvuma baada ya kilio cha muda mrefu cha wakazi wa mkoa huo

Dar es Salaam. Hatimaye Rais John Magufuli amezindua kiwanda cha kuchakata mahindi cha Mlale baada ya kilio cha muda mrefu cha wakazi wa mkoa wa Ruvuma kubaki na mahindi yao kwa kukosa soko.

Hivi sasa wananchi wa mkoa wa Ruvuma wataanza kuuza unga na si mahindi tena waliyokuwa wakidhulumiwa na walanguzi na tayari Rais Magufuli amekata utepe na kuweka jiwe la msingi na kuzindua rasmi kiwanda hicho.

Kiwanda hicho cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mlale kimezinduliwa leo Aprili 8, 2019 ambako Rais Magufuli amesema kitakuwa suluhisho la ukosefu wa soko la mazao kwa wakulima mkoani humo.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenelali Venance Mabeyo amesema kiwanda hicho kimejengwa kwa umahiri mkubwa na JKT.