Magufuli azungumzia ndege ya Tanzania iliyozuiwa Afrika Kusini, atoa onyo

Monday September 16 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi, [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewahakikisha wananchi kuwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), lipo salama na linatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mwezi uliopita ndege ya Tanzania aina ya Airbus A220-300 iliyokodishwa na ATCL ilizuiliwa kuondoka kwa amri ya mahakama ya Guteng katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini baada ya Hermanus Steyn kufungua kesi katika mahakama hiyo akidai fidia ya dola za Marekani Sh33milioni.

Hata hivyo, Serikali ya Tanzania ilishinda kesi hiyo bila kutoa fedha yoyote ambaye aliyeshtaki aliitaka Serikali kuweka fedha dola 33 milioni kama dhamana.

Akizungumza leo Jumatatu Septemba 16, 2019 wakati wa hafla ya uzinduzi wa rada mbili za kuongezea ndege katika uwanja  wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na ule wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rais Magufuli amewatoa hofu wananchi kuhusu mwenendo wa ATCL.

Amesema mradi wa rada hizo utaleta manufaa makubwa ikiwemo kuboresha huduma za ndege hasa katika kipindi hiki Serikali ilivyojizatiti kuimarisha usafiri wa anga nchini ikiwemo kufufuka kwaATCL

“Ndiyo maana mkisikia watu wamekamata ndege msishangae sana ni kwa sababu ATCL inafanya kazi vizuri. Lakini kwangu mimi ni kama kelele za chura ambazo haziwezi kumzuia ng’ombe mwenye kiu kunywa maji.”

Advertisement

“Saa nyingine huwa naukumbuka wimbo wa wasanii wa Kenya wa kundi la ‘Saut Soul’ unaoimbwa wao ‘wakifunika wengine wanafunua’. Sisi tupo hivyo wakijaribu hivi tutafanya hivi ili nchi yetu ifike tulikopanga,” amesema Rais Magufuli.

Amefafanua wakati Serikali inafufua ATCL shirika hilo lilikuwa likishikilia asilimia 3 ya soko la ndani, lakini sasa hivi asimilia 75 pamoja na kuingia katika soko la kimataifa kwa kwenda nchi mbalimbali.

“Safari hizi zitachangia kukuza sekta ya utalii, kwa mafanikio haya lazima watajitokeza watu wenye wivu ambao hawakosekani. Lakini hatutakubali mtu yeyote alichezea shirika hilo na Tanzania lazima tufike tunakotakiwa kufika,” amesema Rais Magufuli.

SOMA ZAIDI

Advertisement