VIDEO: Magufuli azungumzia ujenzi reli ya Tanzania –Rwanda

Muktasari:

Tanzania na Rwanda zinakamilisha mchakato wa ujenzi wa reli itakayounganisha mataifa hayo mawili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mwanza. Tanzania na Rwanda zinakamilisha mchakato wa ujenzi wa reli itakayounganisha mataifa hayo mawili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Reli hiyo itakayounganishwa na ile ya kati itaanzia bandari kavu ya Isaka wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Mradi huo ambao tayari hatua ya upembuzi yakinifu umekamilika utarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari kavu ya Isaka kwenda nchi jirani.

Akizungumza na wananchi wa Isaka leo Jumatano Novemba 27, 2019 Rais wa Tanzania,  John Magufuli amesema kinachoendelea ni kutafuta fedha za utekelezaji.

“Nimeshazungumza na Rais Kagame (Paul wa Rwanda) kuhusu utekelezaji wa mradi huu, upembuzi yakinifu umekamilika. Kinachofanyika sasa ni kutafuta fedha,” amesema Rais Magufuli.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amewataka wakazi wa Isaka kufanya kazi kwa bidii, hasa katika sekta ya kilimo na biashara ili kuzalisha mazao na bidhaa zitakazosafishwa kupitia miundombinu inayojengwa na Serikali.

“Isaka msibakie kukaa mkiangalia haya malori ya mizigo yanayosafirisha mizigo inayohifadhiwa katika bandari kavu, chapeni kazi ikiwemo kutilia mkazo suala la kilimo cha mazao mbalimbali,” amesema Rais Magufuli.

Ametaja mahindi, mpunga na uwele kuwa miongoni mwa mazao yanayoweza kuzalishwa kwa wingi na wakazi wa eneo hilo na Mkoa wa Shinyanga.