Mahakama Tanzania yaelezwa upelelezi kesi ya Kabendera ulipofikia

Monday January 13 2020

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Upande wa Mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari Tanzania, Erick Kabendera umeieleza mahakama wanamalizia uchunguzi katika maeneo yaliyobakia ili kukamilisha upelelezi.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la kutakatisha fedha kiasi cha Sh173 milioni, katika Mahakama ya Hakimu ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali, Ester Martin ameileleza Mahakamani hiyo leo Jumatatu, Januari 13, 2020 wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Martin amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Janeth Mtega upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kwamba wanamalizia vitu vichache ili kukamilisha upelelezi wa shauri hilo.

“Kuna vitu vichache tunamalizia kukamilisha, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa" amedai wakili Martin.

Martin baada ya kueleza hayo, wakili wa Kabendera, Reginald Martine amedai hana pingamizi juu ya maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka.

Advertisement

Hakimu Mtega baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 27, 2020 itakapotajwa.

Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza, Kabendera alifikishwa  Kisutu, Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu, ambayo ni kuongoza genge la Uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha fedha kiasi cha Sh173.2 milioni.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Kabendera anadaiwa kujihusisha na genge la uhalifu, tukio analodaiwa kulifanya katika tarehe tofauti kati ya Januari mwaka 2015 na Julai mwaka 2019, jijini Dar es Salaam.

Katika shtaka hilo, Kabendera anadaiwa  kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia maslahi.

Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo, Kabendera anadaiwa kukwepa kodi, zaidi ya Sh173,247,047.02.

Katika shtaka la tatu, Kabendera anadaiwa, kati ya Januari 2015 na Julai 2019, katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, alitakatisha fedha kiasi cha Sh173,247,047.02.

Advertisement