Mahakama Tanzania yatupilia mbali ombi la Meya Dar

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali ombi la Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita la kuitaka itoe zuio la muda ili asiondolewe kwenye nafasi yake kwa mpaka pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Dar ea Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imetupilia mbali ombi la Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita aliyekuwa anaitaka itoe zuio la muda ili asiondolewe kwenye nafasi yake mpaka pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Uamuzi huo mdogo umetolewa leo Ijumaa Januari 10, 2020 na  Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega.

Akitoa uamuzi huo alisema haikuona uthibitisho mahakamani hapo juu ya uwepo wa kikao cha kumuondoa madarakani Meya huyo wala hasara atakayoipata endapo ataondolewa.

Licha ya kutoa uamuzi huo alipanga kusikiliza kesi ya msingi ya Meya Mwita Januari 13, 2020 ambapo inahusu kupinga mchakato uliyofanyika wa  jana Alhamisi wa kumng'oa katika nafasi yake ambapo ulikiuka utaratibu.

Kwa upande wa kesi ya msingi, Mwita  anapinga kudaiwa kupendelea madiwani wa chama chake katika uundaji wa kamati mbalimbali bila kumshirikisha Mkurugenzi wa Jiji,  kutumia gari la ofisi vibaya na kushindwa kufanya matumizi ya hisa za  Shirika la Usafiri Dar es Salaam  (UDA).