Mahakama ya Tanzania yahitimisha mjadala umri wa kuolewa

Muktasari:

Mahakama ya rufani imetupa rufaa ya Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha vifungu vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.

Dar es Salaam. Mahakama ya rufani imetupa rufaa ya Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyobatilisha vifungu vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Oktoba 23, 2019 baada ya mahakama hiyo kukubaliana na hoja za jopo la mawakili wa mjibu rufaa lililoongozwa na Mpale Mpoki, Jebra Kambole (aliyeshinda kesi ya msingi), Alex Mgongolwa na Fulgence Massawe.

Serikali ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyotokana na  kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwanaharakati na mkurugenzi wa shirika lisilo la Kiserikali la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi.

Jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo lililoongozwa na Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Winfrida Korosso na Dk Mary Lavira, limeithibitisha hukumu hiyo ya Mahakama Kuu, baada ya kutupilia mbali hoja zote za rufaa ya Serikali kuwa hazikuwa na mashiko.

Mahakama ya rufani katika hukumu yake iliyosomwa leo Jumatano Oktoba 23, 2019 na naibu msajili, Fussi imesema kuwa Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kuamua kuwa vifungu hivyo ni vya kibaguzi kati ya mtoto wa kike na wa kiume na havina manufaa yoyote kwa mtoto wa kike.

”Hivyo tunaitupilia mbali rufaa hii yote kutokana na kutokuwa na mashiko,” amesema Fussi akinukuu hukumu hiyo.

Akizungumzia hukumu hiyo Gyumi amesema ni ushindi muhimu kwa watoto wa kike nchini wa kwamba majaji wamesimamia ukweli kwa ujasiri mkubwa.

“Hukumu hii imewapa wasichana wa Tanzania ulinzi wa kisheria waliokuwa wakiukosa kilichobaki sasa ni kuhakikisha hukumu hiyo inatekelezeka haraka ndani ya mwaka mmoja kama ilivyoamriwa tangu awali na Mahakama Kuu,” amesema Rebeca.

Amesema hatua watakazozichukua ni kuendelea kuelimisha jamii kuhusu hukumu hiyo na madhara ya ndoa za utotoni.

Amesema watakaa kujadiliana na kamati za Bunge zenye dhamana na masuala ya sheria kuhakikisha Serikali inawasilisha bungeni haraka muswada wa marekebisho ya sheria hiyo.

Katika kesi ya msingi  namba 5 ya mwaka 2016, Rebeca  alipinga vifungu namba 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa, akidai vinakiuka haki ya mtoto wa kike kupata elimu.

Pia alikuwa akidai kuwa vifungu hivyo ni kinyume cha Ibara za 12, 13, na 18 za Katiba vinavyotoa haki ya usawa mbele ya sheria, kutokubaguliwa, kuheshimu utu wa mtu na haki ya uhuru wa kujieleza.

Mahakama Kuu katika hukumu yake ya Julai 8, 2016 iliyotolewa na jopo la majaji watatu ilikubaliana na hoja za mwanaharakati huyo.

Ilisema vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba kwani mtoto umri chini ya miaka 14 hawezi kuingia katika ndoa maana  hana ufahamu kiasi cha kuweza kujihusisha na mambo ya ndoa.

Pia Mahakama ilisema kuwa vifungu hivyo ni vya kibaguzi kati ya mtoto wa kike ambaye anaweza kuolewa akiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi na mtoto wa kiume ambaye anaruhusiwa kuingia kwenye ndoa akiwa na umri wa miaka 18.

Vilevile ilisema kuwa vinakiuka haki ya kikatiba ya kujieleza kwani ndoa ni uamuzi wa mtu binafsi si wa wazazi au mtu mwingine na iliipa Serikali mwaka mmoja ifanyie marekebisho ya vifungu hivyo na umri wa kuolewa uanzie miaka 18.

Katika rufaa yake iliyosikilizwa Julai 24, 2019  iliwasilisha sababu tano kupinga hukumu hiyo pamoja na mambo mengine mawakili wa Serikali Wakuu, Alesia Mbuya na  Mark Mulwambo waliidai kuwa lengo la vifungu hivyo ni kuwalinda watoto dhidi ya ngono na kupata watoto nje ya ndoa.