Mahakama yaamuru DC Chemba kumlipa mkewe Sh7 milioni

Wednesday September 18 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Ukonga jijini Dar es Salaam imeitupilia mbali kesi ya madai ya talaka iliyofunguliwa na mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga dhidi ya mkewe, Medilina Mbuwuli.

Leo Jumatano Septemba 18, 2019 Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Christina Luguru amesema mkuu huyo wa Wilaya ambaye hakuwepo mahakamani hapo, anatakiwa kutoa Sh7 milioni kama nusu ya gharama za matunzo aliyotumia mkewe kumsomesha mtoto wao kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

Odunga pia ametakiwa kutoa Sh100,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mkewe na mwanaye.

Hakimu Luguru amesema mtoto wao kwa sasa umevuka umri wa miaka 18, hivyo ataamua aishi na nani kati ya wazazi wake hao.

Uamuzi huo umetolewa baada ya hakimu huyo kusikiliza  ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande zote mbili na kuufunga.

Odunga na Mbuwuli walifunga ndoa kanisani na kupata cheti cha ndoa  A no 00140917.

Advertisement

Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Medilina ameishukuru mahakama kwa kutenda haki, akisisitiza kuwa imeandikwa katika vitabu vitakatifu kuwa ndoa iheshimiwe na watu wote.

Ruth Ossoro, aliyefunga ndoa ya serikalini na Odunga ambaye pia alifungua kesi ya kumtaliki na mahakama hiyo kutoa uamuzi kuwa ndoa yao ni batili, amesema uamuzi wa mahakama ni sahihi.

Katika kesi hiyo Odunga aliwakilishwa na baba yake mdogo.

Advertisement