Mahakama yadai Rais wa zamani wa Sudan Omar Bashir alikuwa akipokea mamilioni kutoka Saudia

Muktasari:

Rais Omar al Bashir wa Sudan aling’olewa madarakani na jeshi la nchi hiyo mwezi April mwaka huu.


Khartoum, Sudan.  Upande wa mashtaka wa kesi inayomkabili Rais wa zamani wa Sudan, Rais Omar al-Bashir umedai kuwa kiongozi huyo alikubali kupokea mamilioni ya dola kutoka Saudi Arabia.

Kiongozi huyo ambaye anakabiliwa na mashtaka ya rushwa alifikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Agosti 19 kwa ajili ya kesi yake kusikiliza.

Hata hivyo, mawakili wa kiongozi huyo walidai kuwa tuhuma dhidi ya mteja wao hazina msingi wowote.

Dk Bashir ambaye alitawala Sudan kwa miaka 30 aling’olewa madarakani na jeshi la nchi hiyo mwezi Aprili mwaka huu.

Baada ya mapinduzi hayo Baraza la Mpito la Kijeshi lilishika madaraka jambo lilopingwa kwa maandamano yeliyokuwa na lengo la kudai utawala wa kiraia. Katika maandamano hayo zaidi ya watu 100 waliuawa.

Hata hivyo, Jumapili iliyopita wanaharakati wa demokrasia na viongozi wa jeshi hilo walisaini makubaliano ya kupokezana madaraka mpaka pale uchaguzi mkuu utakapofanyika baada ya miaka mitatu.