VIDEO: Mahakama yaifuta kesi ya Meya wa Dar

Muktasari:

Uamuzi huo umefikiwa baada ya meya huyo kupitia wakili wake kuomba iondolewe bila gharama

Dar ea Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifuta kesi ya  Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita

Kesi hiyo imefutwa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega baada ya Mwita kupitia wakili wake, Hekimwa Mwasipu kuomba iondolewe kwa sababu anaona haina tena maana na kwamba hajapewa haki ya msingi ya kusikilizwa.

Hata hivyo aliomba kesi hiyo iondolewe mahakamani hapo bila gharama kwa kuwa haijafika mwisho.

Kufuatia ombi hilo, wakili wa serikali, Rashid Mohammed hakuwa na pingamizi la kuondolewa kwa kesi hiyo ila aliiomba mahakama iamuru alipe gharama.

Kwa sababu wao walitumia gharama kuhudhuria kwenye kesi hiyo na uandaaji wa majibu waliyokuwa wakiyawasilisha mahakamani hapo.

Kufuatia ombi hilo, Mwasipu alisisitiza kuiomba mahakama kuondoa kesi hiyo bila gharama kwa sababu mteja wake aliiondoa kwa hiari yake mwenyewe na gharama walizotumia upande wa mashtaka ni kodi zao kwa msingi huo aliomba iondolewe pasipo gharama.

Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Mtega alisema mahakama imekubaliana na ombi la kuiondoa kesi hiyo na ikaifuta.

Mwasipu alifikia uamuzi huo baada ya uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo Januari 10, mwaka huu kutupilia mbali ombi la Meya Mwita la kuitaka itoe zuio la muda ili asiondolewe kwenye nafasi yake mpaka pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Katika uamuzi huo mdogo, Hakimu Mtega alisema hakuona uthibitisho mahakamani hapo juu ya uwepo wa kikao cha kumuondoa madarakani Meya huyo wala hasara atakayoipata endapo ataondolewa.

Katika kesi ya msingi, Mwita anapinga kudaiwa kupendelea madiwani wa chama chake katika uundaji wa kamati mbalimbali bila kumshirikisha Mkurugenzi wa Jiji, kutumia gari la ofisi vibaya na kushindwa kufanya matumizi ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda).