Mahakama yaijumuisha TLS kesi kupinga ukomo wa urais

Muktasari:

Mahakama Mkuu imekiunganisha  Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kesi ya kikatiba inayohusu ukomo wa urais iliyofunguliwa na mkulima Patrick Dezydelius Mgoya.

Dar es Salaam. Mahakama Mkuu imekiunganisha  Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika kesi ya kikatiba inayohusu ukomo wa urais iliyofunguliwa na mkulima Patrick Dezydelius Mgoya.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Novemba 18, 2019 na Jaji Benhajj Masoud baada ya kukubaliana na maombi ya TLS. Katika maombi hayo ya TLS, upande wa mashtaka na Mgoya hawakuweka pingamizi.

Oktoba 30, 2019, TLS ilifungua maombi katika mahakama hiyo kuunganishwa katika kesi hiyo huku katika hati ya faragha ya maombi hayo ikieleza kuwa inaomba kuunganishwa kama mdaiwa mwenye maslahi.

Taasisi hiyo ya kisheria inakuwa ya pili kuomba na  kuunganishwa katika kesi hiyo ikitanguliwa na chama cha ACT-Wazalendo.

Leo Jaji Masoud ametoa uamuzi huo akibainisha kuwa pande zote hawakupeleka kiapo kinzani, mahakama haitatoa amri ya kuzuia TLS kuunganishwa katika kesi hiyo.

Amesema kesi ya msingi itatajwa Novemba 22, 2019 saa 3 asubuhi.

Katika kesi hiyo TLS  inawakilishwa na wakili Edson Kilatu. Maombi yake yalisajiliwa 5, 2019 na yalitajwa kwa mara ya kwanza Novemba 11, 2019.

Mgoya alifungua kesi hiyo chini ya kifungu cha 4 cha sheria ya utekelezaji haki na wajibu, sura ya 3 ya mwaka 1994 chini ya Ibara ya 30(3) ya Katiba ya  mwaka 1977.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Mgoya anahoji Ibara ya 40(20 ya katiba ambayo imeweka ukomo wa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano (10) ya uongozi katika nafasi hiyo ya urais.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo itoe tamko na tafsiri ya maana sahihi na athari za masharti ya ibara hiyo.

Pia,  anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana dhahiri ya masharti ya ibara ya 42(2) ya katiba kwa kuhusianisha na masharti ya Ibara za 13,21 na 22 za Katiba hiyo. Vilevile anaiomba mahakama itoe tafsiri ya maana ya ibara hiyo ya 40(2) kwa kuhusianisha na ibara ya 39 ya katiba.

SOMA ZAIDI