Mahakama yamuachia huru Kabendera, alipa fidia na faini

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mwandishi wa habari Erick Kabendera baada ya kulipa faini ya Sh250,000 kwa kosa la kukwepa kodi na  Sh100 milioni kwa kosa la kutakatisha fedha.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru mwandishi wa habari Erick Kabendera baada ya kulipa faini ya Sh250,000 kwa kosa la kukwepa kodi na  Sh100 milioni kwa kosa la kutakatisha fedha.

Mwandishi huyo anatakiwa kulipa fidia ya Sh172 milioni ndani ya miezi sita tangu hukumu iliposomwa leo Jumatatu Februari 24, 2020. Mahakama hiyo imesema hana uwezo wa kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Leo Kabendera  alitiwa  hatiani  baada ya kukiri mashtaka yake mawili ya kukwepa kodi na kutakatisha Sh173 milioni.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega baada ya upande wa mashtaka kumsomea maelezo ya awali ya mshtakiwa huyo.

Kabendera ambaye ni mwandishi wa habari wa kujitegemea alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 5, 2019 akikabiliwa na mashtaka matatu.

Leo amefutiwa shtaka la kuongoza genge la uhalifu na kubaki na mashtaka mawili ya  kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh173.2 milioni ambayo alikutwa na hatia.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi