Mahakama yamuonya Zitto

Muktasari:

Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe akitarajiwa kuanza kujitetea Machi 17, 2020 baada ya kukutwa na kesi ya kujibu,  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka kuhudhuria mahakamani hapo kila kesi yake itakapotajwa.

Dar es Salaam. Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe akitarajiwa kuanza kujitetea Machi 17, 2020 baada ya kukutwa na kesi ya kujibu,  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka kuhudhuria mahakamani hapo kila kesi yake itakapotajwa.

Onyo hilo limetolewa leo Jumanne Februari 18, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi muda mfupi baada ya Zitto kukutwa na kesi ya kujibu katika mashtaka matatu ya uchochezi yanayomkabili.

Hakimu Shaidi amesema mshtakiwa anapokuwa na kesi mahakamani anatakiwa kuhudhuria, kufuata taratibu zote zinazowekwa bila kujali wadhifa wake.

Amebainisha kuwa kesi hiyo ilipotajwa mara ya mwisho mahakamani hapo, Zitto hakuwepo na taarifa zake kutolewa na mtu mwingine aliyekuwa ameongozana naye katika safari yake nje ya nchi.

"Kwa sababu mshtakiwa amehudhuria  mahakamani bila kukamatwa imesaidia, jambo la msingi ni kuhudhuria kesi yake kila mahakama inapopanga tarehe,” amesema Hakimu Shaidi.

Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka akisaidiana na wakili wa Serikali mwandamizi, Nasoro Katuga amedai kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kusomewa uamuzi kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Katuga alikumbusha kuwa tarehe iliyopita, mahakama ilipanga mshtakiwa kujieleza  lakini hakufika mahakamani huku taarifa zake zikitolewa  na mtu mwingine.

Pia alihoji uhalali wa nyaraka ya matibabu iliyotolewa mahakamani na Zitto, kwamba haina muhuri  wa hospitali aliyotibiwa kama zinavyokuwa nakala halisi za namna hiyo.

Zitto alitoa nyaraka hiyo kuithibitishia mahakama kuwa alikuwa nje ya nchi na alishindwa kuhudhuria kesi yake baada ya kuugua. Alieleza kuwa alipatiwa matibabu katika hospitali ya Leesburg iliyopo Virginia nchini Marekani.

Katika majibu yake, Zitto amesema aliugua alipokuwa nje ya nchi na waliokuwa wamesafiri naye walitoa taarifa kwa wakili na kwa mdhamini wake.

"Kwa hali niliyokuwa nayo nilishauriwa na daktari kumueleza yule niliyesafiri naye atoe taarifa kwa wakili wangu na wadhamini wangu,” amesema.

Alipohojiwa kama ana utambulisho wowote unaoashiria kuwa alikuwa akipatiwa matibabu, Zitto alidai kuwa na barua ya matibabu na kisha kuitoa.

Alipoiona barua hiyo wakili Kweka amesema haieleweki, haina anuani wala muhuri wa hospitali, “pia barua hii inaonyesha mshtakiwa alipokelewa hospitali hapo Februari 8 na kuanza matibabu siku hiyohiyo, lakini upande wa mashtaka tulitaka mshtakiwa awasilishe barua ambayo ni halisi na sio kopi, hivyo tuna wasiwasi na nyaraka hii, mtu  yoyote anaweza akaitengeneza.”

Alijibu hoja hiyo, Zitto amesema hiyo ni barua ya kikazi na ina  anuani, kama mawakili wa Serikali hawaamini wawasiliane na ubalozi wa Marekani kwa ajili ya kupata ufafanuzi kuhusu nyaraka hiyo.

"Naamini upande wa mashtaka hawajawahi kukutana na nyaraka kama hiyo, mimi ni mbunge na mwakilishi wa wananchi, siwezi kufanya vitu ambavyo havina maana,” amedai Zitto.

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Shaidi amesema barua ya mshtakiwa haina muhuri lakini kwa kuwa amefika mahakamani bila kukamatwa, anatakiwa kuzingatia utaratibu unaowekwa na mahakama  kuhudhuria kesi kila tarehe inayopangwa.

Baada ya maelezo hayo kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 17 hadi 20, 2020. Siku hizo tatu Zitto atajitetea.

Katika maelezo yake Zitto amesema atajitetea na atakuwa na mashahidi 10. Tayari mashahidi 15 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi.