VIDEO: Mahakama yaruhusu Dk Tenga, wenzake kuteta na jopo la mawakili wao

Tuesday September 24 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imeridhia ombi la upande wa utetezi la kutaka kuja kuzungumza na wateja wao mahakamani, Ijumaa ya Septemba 27, 2019.

Ni katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo watano wa kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili maarufu nchini humo, Dk Ringo Tenga.

Dk Ringo ambaye ni Mkurugenzi na Mwanasheria wa Kampuni hiyo na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22.

Ombi hilo limetolewa leo Jumanne Septemba 24, 2019 na wakili anayewatetea  washtakiwa hao, Alex Mgongolwa wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Mgongolwa ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba kuwa wanaomba kuja kuzungumza na wateja wao Ijumaa ya wiki hii.

"Najua kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa, ila sisi upande wa utetezi tunaombi, tunaomba kesi hii uipange Septemba 27, mwaka huu ili tuje tuzungumze na wateja wetu (washtakiwa) mahakamani hapa" amedai Mgongolwa.

Advertisement

Wakili Mgongolwa baada ya kueleza hayo, upande wa mashtaka umedai hauna pingamizi dhidi ya ombi hilo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, amekubaliana na ombi la upande wa utetezi na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 27, 2019 kesi hiyo itakapotajwa.

Awali, wakili wa Serikali Constantine Kakula ameeleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Novemba 20, 2017 wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa hao ni  Alex Mgongolwa, Semi Malima, Constancia Sospeter, Jeremiah Mtobesya na Bryson Shayo.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo na wenzake wanadaiwa kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14,2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa  chini ya kiwango cha Dola za Marekani  0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya TCRA kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao, wanadaiwa  katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashtaka yaliyotangulia.

Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22.

 

Advertisement