Mahakama yasema Bunge ruksa kusaka rekodi za kodi za Trump

Washington. Mahakama ya Rufani nchini Marekani imesema Bunge liko huru kuagiza nyaraka za kodi za Rais Trump kwa karibu miaka kumi.

Hilo ni pigo jipya kwa kiongozi huyo ambaye amekuwa akipambana kuhakikisha rekodi zake haziangukii mikononi mwa wapinzani wake wa Democrats.

Hii ni mara ya pili kwa Trump kukwama katika Mahakama kuu katika jaribio la kuzuia wito wa bunge wa kutaka nyaraka za zaidi ya miaka minane ya ulipaji wake wa kodi.

Baada ya uamuzi huo, Wakili wa Trump, Jay Sekulow palepale ametangaza kuwa jopo la wanasheria wa Trump litakata rufaa katika Mahakama ya Juu.

Majaji katika Mahakama ya Rufani waliyakataa maombi ya Trump ya kutaka kusikiliza upya uamuzi uliofanywa na majaji watatu mwezi uliopita.

Katika uamuzi huo wa Oktoba walikataa maombi ya Trump kwa majaji wawili kukayataa na mmoja akiyakubali, kwamba kamati ya Bunge haikuwa na mamlaka ya kumtaka rais kuwasilisha nyaraka za kodi za muda mrefu.

Bunge linalotawaliwa na Democrats linataka nyaraka za ulipaji kodi wa Trump kati ya 2011 na 2018, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa biashara zake kwa kuwa aliahidi kwenye kampeni kuwa angetoa rekodi hizo.

Wanasheria wanataka kubaini iwapo Trump alipandisha thamani ya mali zake ili kupata mikopo.

Katika wito wa Bunge wa Aprili, Trump alitakiwa kuwasilisha taarifa za hali ya kifedha, ripoti za mwaka na kila mara za fedha, ripoti za ukaguzi huru wa hesabu na ule uliofanywa na kampuni ya kimataifa ya Mazars.

Ikulu ya Marekani ambayo imeueleza uchunguzi huo kama unyanyasaji kwa rais, imesema Bunge halihitaji nyaraka hizo kwa ajili ya kufanikisha majukumu yake kama chombo cha kuitunga sheria.

Mmoja wa wagombea wa Demokratic katika uchaguzi mwaka 2020, Joe Biden alifurahia uamuzi wa Mahakama ya Rufani, akisema kupitia Twitter, kuwa Wamarekani anapaswa kujua “Trump anachoficha katika nyaraka za kodi.”

Uamuzi huo ni pigo jingine kwa Trump baada ya Democrats jana Jumatano kuanzisha uchunguzi wa kina na wazi wenye lengo la kumng’oa madarakani.