Mahakama yataka kesi ya kigogo Takukuru itendewe haki

Monday October 21 2019

 

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected], co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haki itendeke katika kesi ya kumiliki mali ya zaidi ya Sh3.6 bilioni kinyume na kipato halali inayomkabili aliyekuwa Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),Godfrey GugaI na wenzake wawili kwa kuwa washtakiwa hao hawana dhamana.

Wakili wa Serikali Sylvia Mitanto amedai leo Jumatatu Oktoba 21, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini wakili anayeendesha shauri hilo amepata udhuru.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba amesema kesi hiyo lazima itendewe haki kwa kuwa washtakiwa hawana dhamana.

“Lazima kesi hii itendewe haki kwa kuwa washtakiwa hawana dhamana,” amesema Hakimu Simba

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 28, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Mbali na Gugai, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga na Leonard Aloys.

Advertisement

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 39 kati ya hayo 20 ya utakatishaji wa fedha na 19 ya kugushi. Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba, 2015.

Advertisement