Mahakama yataka uthibitisho afya ya Tundu Lissu

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewataka wadhamini wa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwenda na uthibitisho wa maendeleo ya afya yake kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewataka wadhamini wa aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kwenda na uthibitisho wa maendeleo ya afya yake kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Oktoba 23, 2019 baada ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba kuuliza maendeleo ya Lissu na mdhamini wa mwanasheria mkuu huyo wa Chadema, Robert Katula kudai kuwa Lissu bado anaumwa.

Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na sheria ya magazeti ya mwaka 2002.

Septemba 7, 2017 Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma kisha usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alitibiwa hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa nchini Ubelgiji kukamilisha matibabu.

Leo mahakamani baada ya maelezo ya mdhamini wa Lissu, wakili wa Serikali, Estazia Wilson alieleza kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa, hawawezi kuendelea na watamsubiri Lissu hadi afya yake itakapoimarika.

Baada ya maelezo hayo hakimu Simba amesema shauri hilo litakapotajwa tena mahakamani hapo mdhamini wa Lissu anatakiwa kuja na uthibitisho wa maendeleo ya mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki.

"Mdhamini wa Lissu utatuletea uthibitisho wa afya ya Lissu ili tuweze kuweka kwenye rekodi zetu," amesema  Simba na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21, 2019.

Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni mhariri wa gazeti la Mawio,  Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

                : Tundu Lissu akwamisha kesi yake kuendelea

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13 ,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa msajili wa magazeti.