Mahakama yawataka kina Mbowe kujitetea kwa siku tatu

Monday October 21 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe watajitetea kwa siku tatu katika kesi ya jinai namba 112 ya 2018.

Viongozi hao watajitetea kuanzia Novemba 4, 5 na 8, 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba ametoa uamuzi huo mdogo leo Jumatatu Oktoba 21, 2019 mbele ya mawakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya, Hekima Mwasipu na mawakili wa Serikali, Faraja Nchimbi, Wankyo Simon na Salim Msemo.

Hakimu Simba akitoa uamuzi huo amesema wiki tatu zilizoombwa na upande wa utetezi ni nyingi  hivyo aliwapatia wiki mbili ili waweze kuwaandaa washtakiwa waanze kujitetea kabla ya mashahidi wao

Hakimu Simba amesema mashahidi katika kesi hii mbali na washtakiwa ni wengi kweli  200 upande wa utetezi wanahitaji kupewa muda wa maandalizi.

Lakini huo muda wa wiki tatu ulioombwa na upande wa utetezi, mahakama inaona huo muda ni mrefu kwa mazingira ya kesi hiyo na namba ya mashahidi iliyowaita, aliwapatia muda wa wiki mbili ili waweze kujiandaa na utetezi.

Advertisement

Kuhusu kielelezo namba 5  ambacho ni video ya maandamano kilichoombwa na upande wa utetezi ili wataalam wao wakichunguze kwa sababu wana wasiwasi kimehaririwa, Hakimu Simba alisema 

 

watakitumia kupitia vifaa vya  mahakama vile vile vilivyotumiwa na upande wa mashtaka.

 

Hata hivyo, watakuwa chini ya usimamizi wa mtendaji wa mahakama ili kuangalia usalama wa jengo, vielelezo na vifaa vitakavyotumiwa na kwamba upande wa utetezi utoe taarifa kwa mahakama siyo chini ya siku tatu ili maandalizi yafanyike.

"Kutoka na wingi wa mashahidi hakuna namna kusikiliza kesi hii mfululizo na ni lazima isikilizwe mfululizo itaanza Novemba 4,5 na 8, 2019" alisema Hakimu Simba. 

Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo baada ya ya Oktoba 18, 2019, Wakili wa utetezi Peter Kibatala kuomba wapatiwe muda wa wiki tatu ili waweze kuandaa washtakiwa na mashahidi wao kwa utetezi.

 

Awali, Kibatala aliieleza mahakama kuwa washtakiwa hao watatoa ushahidi wao chini ya kiapo kwa kadri dini zao zinavyoruhusu.

 

 

Washtakiwa hao wanaanza kutoa utetezi wao baada ya mashahidi  nane wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao na Mahakama kuwaona washtakiwa hao wana Kesi ya kujibu wajitetee.

Wanaokabiliwa katika kesi hiyo,  mbali Mbowe ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar-Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji.

Wengine ni wabunge; John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Esther Matiko (Tarime Mjini).

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendajia jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam

Advertisement