Maiti ya mama, mwanaye zahifadhiwa siku 12 Muhimbili bila kutambuliwa

Muktasari:

Maiti mbili za ajali ya gari iliyotokea Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani Agosti 31, 2019 na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), zimefikisha siku 12 bila kutambuliwa na ndugu.

Dar es Salaam. Maiti mbili za ajali ya gari iliyotokea Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani Agosti 31, 2019 na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), zimefikisha siku 12 bila kutambuliwa na ndugu.

Maiti hizo zilizotambuliwa kuwa ni mama na mwanaye baada ya vipimo vya vinasaba (DNA), ni kati ya tano zilizopelekwa katika hospitali hiyo zikiwa zimeharibika kutokana na kuungua baada ya gari ndogo kugongana na lori la kampuni ya Dangote.

Ofisa uhusiano wa MNH,  Sofia Mtakasimba amewataka ndugu kujitokeza kutambua maiti hizo kwa kuwa zimekaa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji,  Onesmo  Lyanga baada ya magari hayo kugongana lori hilo lilipoteza mwelekeo na kugonga nguzo ya umeme na nyaya kuanguka na kusababisha moto.

Amesema  gari dogo likiwa na watu wawili liliingia barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda Mtwara bila kuzingatia sheria na kugongana na lori hilo lililokuwa na watu sita.

Septemba Mosi, 2019  MNH ilitoa wito kwa ndugu kujitokeza kupima DNA ili kutambua miili kabla ya kuzikwa ndipo walipojitokeza ndugu wa maiti tatu.

Waliotambuliwa ni Zahoro Gombo, Feruzi Sukari na Cadwell Msambwa ambao wote maiti zao zimeshachukuliwa.

Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa MNH, Dk Pracesa Ogweyo amesema wanahifadhi miili isiyo na ndugu kwa kati ya siku 14 hadi 21 kabla ya kuwakabidhi Halmashauri ya Jiji kwa ajili ya maziko.