Majaliwa: Ahadi zote zilizotolewa na Rais Magufuli zitatekelezwa

Muktasari:

Ziara ya siku tano ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa mkoani Morogoro inahitimishwa leo Jumatano ambapo jana Jumanne aliwaeleza wakazi wa mkoa huo kwamba ahadi zote zilizotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 zitatekelezwa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ahadi zote zilizotolewa na Rais wa nchi hiyo, John Magufuli ikiwemo ujenzi wa barabara ya Mikumi- Ifakara kwa kiwango cha lami zitatekelezwa hivyo amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali yao.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Waziri Mkuu leo Jumatano Septemba 18, 2019 imesema Majaliwa alisema hayo jana Jumanne wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Mji wa Ifakara mkoani Morogoro pamoja na wilaya ya Kilosa alipokuwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

“Kila alichokiahidi Mheshimiwa Rais John Magufuli nitakisimamia kuhakikisha kinatekelezwa, hivyo wananchi endeleeni kuiamini Serikali yenu.”

“Serikali yenu ipo makini na ina dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo kama Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2015-2020 inavyoelekeza,” alisema

Waziri Mkuu alisema Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli iko makini na inaendelea kuchapa kazi kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini yakiwemo na mkoa wa Morogoro.

Pia, Majaliwa alisema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini.

Alisema iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema watumishi wa umma wanapaswa kuwa na nidhamu ya fedha za Serikali zinazopelekwa katika maeneo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ya afya, elimu na maji na, “Sina mzaha na watakaotafuna fedha hizo.”